Dar es Salaam. Migogoro ya kifamilia haichagui jinsia, kwani hata wanandoa wenye umri wa zaidi ya miaka 65 wanaweza kukutana na changamoto zinazoweza kuvunja ndoa zao.

Hii ndio iliyoibuka kwa mwanandoa mmoja jijini Dar es Salaam, ambapo baba alidai kunyanyaswa na kudharauliwa ndani ya nyumba yake.

Mgogoro huo ni miongoni mwa mashauri 49 yaliyopelekwa katika Kliniki ya Sheria, iliyozinduliwa Februari 16, 2026, Mnazimmoja, jijini Dar es Salaam, ikilenga kusaidia wakazi kwa masuala ya kisheria bila malipo.

Mashauri hayo, yaliyosikilizwa hadi Februari 20, 2026, yamehusisha mgawanyo wa mali baada ya ndoa, matunzo ya watoto, unyanyasaji wa kijinsia na vipigo.

Akizungumza Februari 21, 2026, Wakili wa Serikali, Fatma Pangalugome amesema shauri la wanandoa hao lilifika Februari 18, 2026, kutoka kwa mama aliyemfuata wakili akiomba msaada kisheria, baada ya mumewe kumtenga kwa miaka minne, akidai hakupata matunzo wala amani nyumbani.

“Siku hiyo alikuja mama akilia, akasema mume wake amejitenga, hampi matumizi, hampi chakula na ameamua kulala chumba kingine. Akaomba nimsaidie kurejesha ndoa yake,” amesema Fatma.

Fatma amesema baada ya kumwandikia mume barua ya wito, alikubali kufika Februari 19, 2026.

Kikao kilianza kwa mama kueleza changamoto zake, lakini hali ilibadilika baada ya baba kupewa nafasi ya kueleza upande wake.

Baba alieleza kuwa chanzo kikubwa cha mgogoro kilikuwa ukosefu wa mipaka na heshima, huku watoto wakubwa wakiingia chumbani kwa wazazi bila utaratibu.

Aidha, alilalamika kutoheshimiwa na kumnyanyasa mtoto wake wa nje ya ndoa, jambo lililosababisha kujitenga na mkewe.

Baba pia alikiri kuwa licha ya kutoa fedha za familia na kusaidia miradi yao, mkewe hakutimiza majukumu yake kikamilifu.

Hali hiyo ilisababisha baba kulala chumba kingine na kusitisha baadhi ya majukumu kama ishara ya kutoridhishwa kwake.

Baada ya kusikiliza pande zote, wakili aliwashauri wanandoa kuhusu umuhimu wa mawasiliano, heshima na mipaka kwa watoto bila kujali uhusiano wao wa kuzaliwa.

Mume alikubali kurejea chumbani na kuanza upya, huku mama naye akikiri makosa na kuahidi kushirikiana.

Baba pia amekubali kumpa mkewe nyumba moja binafsi kwa usimamizi wa mambo yake.

Siku hiyo hiyo, wanandoa walirejea nyumbani pamoja na kuanza maandalizi ya kuhamia chumba kipya.

Watoto walialikwa kufanya kikao cha familia kuweka misingi mipya ya heshima na maadili.

“Wamenipigia simu wakiwajumuisha watoto wote, tayari wamefika kwa mazungumzo na nimepewa mrejesho unaotarajiwa kuleta faraja ndani ya familia,” amesema Fatma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *