Dar es Salaam. Mkazi wa Mhero, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Youze Kituo na wenzake sita wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Same wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha kilo 137.8 za mirungi, huku mmoja wao akiwekwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi kwa miaka mitatu.

Mbali na Kituo, washtakiwa wengine ni Athuman Kivuma, Nuru Mndeme, Edson Kibaja, Goodluck Mungulu, Ahadi Mnjama na Mganga Dorovu, ambao wote ni wafanyabiashara na wakazi wa Same.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo jana Februari 19, 2026 na kusomewa mashtaka yao na mahakimu wawili tofauti.

Katika kesi ya kwanza, Kivuma, Mungulu na Nuru wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Jackson Matowo, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Christanta Chitanda.

Akiwasomea mashtaka yao, Wakili Matowo alidai washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 11, 2026 katika maeneo ya Indini, Marieni na Kitahiro yaliyopo katika Kata ya Chome, Wilaya ya Same.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa Kivuma alikutwa akisafirisha kilo 27 za mirungi; Mungulu kilo 1.8 za mirungi na Mndeme kilo 25.

Washtakiwa wamekana kutenda kosa hilo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 24, 2026 kwa ajili ya kusomewa hoja za awali baada ya upelelezi kukamilika.

Hata hivyo, mshtakiwa Mungulu shtaka lake lina dhamana, ila ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana, huku washtakiwa wenzake wakiwa hawana dhamana.

Kwa upande wake, mshtakiwa Kituo, Mnjama na Kibaja wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Hellen Hozza.

Wakili Matowo alidai washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 11, 2026 katika eneo la Mhero lililopo Kata ya Chome, Wilaya hiyo.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa Kituo alikutwa na kilo 34 za mirungi, Mnjama kilo 26 na Kibaja kilo 24.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao walikana na kesi zao zimeahirishwa hadi Machi 2 na Machi 3, 2026 kwa ajili ya kusomewa hoja za awali.

Wakati huo huo, Mahakama hiyo imeamuru mshtakiwa wa saba katika kesi hiyo, Mganga Dorovu, kuwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi kwa kipindi cha miaka mitatu na kuripoti kituoni kila mwezi.

Uamuzi huo unatokana na upande wa Jamhuri kuwasilisha maombi ya mshtakiwa huyo kuwa chini ya uangalizi wa Polisi.

Pia mshtakiwa huyo amepewa masharti mengine ya kutojihusisha na uhalifu wowote, ikiwemo biashara au matumizi ya dawa za kulevya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *