Licha ya vizuizi vikali vilivyowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel vya kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa, makumi ya maelfu ya Wapalestina jana usiku walihudhuria katika msikiti huo mtukufu kusali Sala za I’sha na Tarawehe wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina Ma-a’a, Idara ya Wakfu wa Kiislamu katika mji wa Baitul-Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu imetangaza kuwa, waumini Wapalestina 100,000 walihudhuria kwenye Msikiti wa Al-Aqsa jana usiku kutekeleza ibada ya Sala na I’sha na Tarawehe.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mahudhurio makubwa ya Wapalestina katika Msikiti wa Al-Aqsa yanashuhudiwa wakati utawala wa Kizayuni umeweka vizuizi vikali mwaka huu kwa waumini hao kuingia katika eneo hili takatifu.

Maghasibu wa Kizayuni wamewazuia wakazi wa Ukingo wa Magharibi kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa na kuwarudisha maelfu miongoni mwao kutokea kituo cha ukaguzi cha Qalandiya kilichoko kaskazini mwa Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu.

Siku ya Ijumaa, Sheikh Ikrimah Sabri, Khatibu wa Msikiti wa Al-Aqsa, alieleza katika mahojiano na Al Jazeera kwamba tangu mwezi mmoja nyuma, utawala wa Kizayuni umekuwa ukipanga kuwawekea vizuizi waumini wakati wa mwezi wa Ramadhani.

Alisema: “Vikosi vya utawala ghasibu, vinatumia visingizio vya kiusalama, ili kuzuia kile kisichovipendeza, yaani mahudhurio makubwa ya maelfu ya Waislamu katika Msikiti wa Al-Aqsa; na lengo la mipango hiyo ni kupunguza idadi ya Waislamu katika mji wa Quds na mahali hapa patakatifu.”

Khatibu huyo Msikiti wa Al-Aqsa amesisitiza: “Hatua na vizuizi vilivyowekwa mwaka huu vimekuwa vikali zaidi na vya kuchochea mivutano zaidi kuliko ilivyokuwa katika miaka iliyopita”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *