Shinyanga. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amewaonya vijana kuwekeza muda wao vizuri na kuchangamkia kila fursa inayowezekana, akisisitiza kuwa mafanikio hayawezi kutegemea huruma bali jitihada binafsi.

Amesema hayo leo, Februari 21, 2026, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana la Mkoa wa Shinyanga, lililofanyika Manispaa ya Shinyanga.

Nanauka amebainisha kuwa kila kijana anapaswa kuwa na ndoto, kuanza kujisaidia mwenyewe na kuweka malengo ya kile anachotaka kufanikisha.

“Kila mtu anaona kile anachokiwaza. Kwa hivyo, usubiri huruma hakutasaidia; bali jitihada zako, muda uliowekeza na mipango thabiti ndizo zitakazokuwezesha kufanikisha ndoto zako,” amesema Nanauka.

Aidha, Waziri amebainisha mambo matatu muhimu kwa vijana kufanikisha maisha yao: kwanza, kupanga muda wao vyema; pili, kuwekeza kwenye elimu, ujuzi na mafunzo; na tatu, kujitahidi kuanzisha miradi midogo ya kiuchumi itakayowasaidia kujipatia kipato na kujenga msingi thabiti kwa kesho bora.

Jukwaa hilo limewaleta pamoja vijana kutoka manispaa na wilaya mbalimbali wa Mkoa wa Shinyanga, ambapo wamepata fursa ya kupata mafunzo, ushauri wa kielimu na kiuchumi, na kuzungumza kuhusu changamoto zinazowakabili katika kujiletea maendeleo binafsi.

“Kesho la vijana inaanzia leo. Kila mmoja anapaswa kuanza safari ya kujisaidia mwenyewe na kuwekeza muda wake vyema. Fursa hazina huruma, bali zinapatikana kwa wale wanaochukua hatua,” amesema huku akiwahimiza vijana kushirikiana na kuendelea kujenga uwezo wa kuanzisha miradi midogo na kuendeleza maisha yao.

 “Maisha hayamfanikishi mtu kwa kumwonea huruma kwa sababu jambo unalotakiwa kulifanya asubuhi usiache kulifanya sababu unaweza usilifanye tena ukabaki unalaumu watu kwa kutokukusaidia, tunatatikwa kuwekeza kwenye muda na kuambatana na watu wenye fikra chanya na kuwa na msimamo wa kile unachotaka kukifanya sababu mtu wa kwanza kuzuia mafanikio yako ni wewe mwenyewe” amesema Nanauka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema kuwa kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, Mkoa wa Shinyanga una zaidi ya vijana 697,756.

Mhita amesisitiza kuwa mkoa unatambua umuhimu wa vijana katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, uvuvi, ufugaji, uchimbaji madini, na biashara ndogo ndogo, na kwamba ni lazima vijana wachangamkie fursa hizi kwa kuendeleza uwezo wao wa kiuchumi na kujijenga kimaslahi.

 “Mkoa umeweka mazingira rafiki kwa vijana wajasiliamali kusajiliwa katika mfumo wa kielektroniki na vijana 2,453 wamesajiliwa, huku wasichana ni 1,334 na wanaume 1,119 na Benki ya NMB imetoa Sh255 milioni kwa vijana wanufaika 124 wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali, pia kwa mwaka 2024/2025 halmashuri zimetoa zaidi ya Sh2 bilioni  ya mikopo ya asilimia 10,” amesema Mhita.

Ameongeza kuwa, “Bilioni 5 (Sh5 bilioni) zimetengwa kwa ajili ya vijana wanajihusisha na mambo ya sanaa kama, uchoraji, muziki wa kizazi kipya na nyimbo za asili, DJs, MCs, uigizaji na sanaa zingine ikiwemo ubunifu,” ameongeza Mhita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *