Dar es Salaam. Huu ndiyo mwisho wa zama za Profesa Ibrahim Lipumba. Ndivyo unavyoweza kuelezea mfululizo wa matukio yanayoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kueleza kutoutambua uongozi wake.

Februari 14, 2026, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilibatilisha uchaguzi mkuu uliomweka madarakani Profesa Ibrahim Lipumba na viongozi wenzake watano, ukiwa umepita mwaka mmoja tangu ulipofanyika.

Mbali na Profesa Lipumba, wengine walioathirika na uamuzi huo ni makamu wenyeyekiti, Mbarouk Seif Salim (Zanzibar), Othman Dunga (Bara), Katibu Mkuu, Husna Mohamed Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya (Bara) na Ali Juma Khamis (Zanzibar).

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama Cha Wananchi (CUF), wakati wa uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho.

Sababu ya kubatilishwa kwa uchaguzi huo uliowaweka madarakani ni kuwa washindi hawakupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa na wajumbe, kinyume na matakwa ya katiba ya chama inayohitaji mshindi kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura halali.

Hata hivyo, hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, waliowasilisha pingamizi Desemba 19, 2024 katika Ofisi ya Msajili wakidai kuwapo kwa ukiukwaji wa katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi katika mchakato uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024 uliomweka madarakani Profesa Lipumba na wenzake.

Wajumbe waliowasilisha malalamiko hayo ni Maftaha Nachuma, Fatuma Athuman, Khamis Khamis Ameir, Ismail Issa Chitutuli, Zuwena Kitatichingi, Liwikula Omari Mohamed, Kassim Mossi Ameir na Ruwaid Abdala Kassim, wakipinga mchakato huo kwa madai ya ukiukwaji wa katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi katika uchaguzi mkuu wa chama chao uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024.

Uamuzi huo wa Msajili umeitikisa ngome ya Profesa Lipumba ambaye amekiongoza chama hicho kwa takribani miongo mitatu, akiwa mwenyekiti wa CUF. Hata alipoandika barua ya kujiuzulu mwaka 2015, alirejea tena madarakani mwaka uliofuata.

Kurejea kwa Profesa Lipumba madarakani kuliibua mgogoro mwingine ndani ya chama ambao ulisababisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kutimkia ACT Wazalendo baada ya Mahakama Kuu kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa CUF.

Tangu Msajili alipotangaza uamuzi huo na kutoa maelekezo ya uchaguzi kurudiwa, chama hicho kimepeleka mambo haraka haraka, kuanzia kikao cha Baraza Kuu, mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu, uteuzi wa wagombea hadi mkutano mkuu unaochagua viongozi.

Kikao cha Baraza Kuu

Chama hicho kimeanza kutekeleza maagizo ya Msajili ya kurudia uchaguzi huo ambapo umeibua pande mbili ndani ya chama; upande wa Profesa Lipumba ambao unakusudia kwenda mahakamani, na upande wa walalamikaji ambao ndiyo wamepokea kwa furaha uamuzi huo.

Jana, Februari 20, 2026, kikao cha Baraza Kuu la CUF kilifanyika makao makuu, Dar es Salaam, ambapo baada ya akidi kutimia, kikao kilianza mara moja. Hata hivyo, siyo Profesa Lipumba wala watu wake wa karibu walioshiriki kikao hicho.

Kikao hicho kilipitisha uamuzi wa kufungua dirisha la uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa makada wa CUF wanaotaka kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi tatu za juu ndani ya chama hicho, ikiwemo nafasi ya mwenyekiti wa Taifa.

Kwa mujibu wa Baraza hilo, ambalo wakati fulani liligubikwa na vurugu, kelele na baadhi ya wajumbe kujikuta mikononi mwa polisi na kutolewa nje ya ukumbi baada ya fomu kurejeshwa, kutafanyika kikao cha dharura cha kufanya mchujo wa majina.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama Cha Wananchi (CUF), wakati wa uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho.

Watakaokidhi vigezo kwa mujibu wa Katiba na taratibu za chama watakwenda kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu wa dharura unaotarajiwa kufanyika kesho katika Ukumbi wa Lekham, mkabala na ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni.

Majina matatu yapitishwa

Leo, Februari 21, 2026, kikao cha Baraza Kuu kimeendelea ambapo shughuli ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu iliendelea, ambapo makada 20 walijitokeza kuchukua na kurejesha fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Wakiwa wamevalia kofia zenye picha ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, wajumbe wa kikao hicho walipokea taarifa na kusomewa majina ya makada waliorejesha fomu kabla ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Mbali na kutoshiriki kikao hicho, Profesa Lipumba siyo miongoni mwa watu waliochukua na kurejesha fomu kuwania nafasi hiyo, jambo linaloashiria mwanzo wa kustaafu kwake katika nafasi yake ndani ya CUF.

Baraza hilo limepitisha majina matatu kwa nafasi ya mwenyekiti ambayo ni Othman Omar Dunga, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa CUF Tanzania Bara, Mirambo Camil Yusuf na Nkunyunyika Siwale.

Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, waliopitishwa ni Mussa Mbarouk, Mohammed Ngulangwa na Miraji Mtibwiliko, wakati Makamu Mwenyekiti Zanzibar wakiwa ni Haroub Mohamed Shamsi, Mbarouk Seif Salim na Amina Rashid Salim.

Majina hayo yamepatikana baada ya kukamilika kwa kikao cha dharura cha wajumbe, kilichofanya mchujo na kupitisha majina ya makada 20 waliochukua na kurejesha fomu hizo zilizotolewa bure kuanzia jana mchana kuwania nafasi hizo tatu za juu za uongozi CUF.

Baada ya kupatikana kwa majina hayo, yatawasilishwa kwenye mkutano mkuu wa chama unaoendelea katika Ukumbi wa Lekham, mkabala na ofisi za chama hicho, Buguruni, jijini Dar es Salaam, na wajumbe wa mkutano huo watamchagua mwenyekiti mpya na wasaidizi wake.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa mchujo huo, mwenyekiti wa kikao hicho, Haroub, amesema orodha hiyo itawasilishwa kwa wajumbe ili wapate fursa ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.

“Tumekamilisha mchujo na kwa kila nafasi tumepitisha majina matatu. Sasa tunaelekea ukumbini ambako wajumbe wanasubiri ili kuanza mchakato wa kupiga kura, ambapo kwa kila nafasi atapatikana mshindi mmoja,” amesema.

Wajumbe watoa ya moyoni

Mohamed Said, kada na mjumbe wa mkutano mkuu wa CUF, amesema mchakato huo ni mwisho wa enzi za utawala wa mwenyekiti wao wa muda mrefu, Profesa Lipumba huku akisisitiza kuwa sasa atakuwa mjumbe wa kawaida wa kudumu.

“Hatakuwa kiongozi tena; sasa atakuwa mwanachama wa kawaida na kiongozi mstaafu wa chama. Ataendelea kuheshimiwa kama viongozi wengine waliokiongoza chama hiki kwa muda mrefu na kufanya makubwa,” amesema.

Amesema kutokuwepo kwa Profesa Lipumba katika nyadhifa za juu ndani ya chama hicho hakuwezi kusababisha madhara yoyote, kwani tangu chama hicho kuanzishwa mwaka 1992 kimepitia panda na shuka nyingi, lakini kimeendelea kustahimili kulingana na nyakati.

“Ukiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM), CUF kilipata usajili wa kudumu namba mbili; hivyo tumefanya mengi katika kupigania haki, na tumekuwa na viongozi bora, ingawa hatuwezi kuwalinganisha,” amesema.

Kwa upande wake, Haroub Mohamed Shamsi, aliyewahi kuwa mbunge kupitia chama hicho, amesema kufanyika kwa uchaguzi huo kunaashiria mwisho wa uongozi wa Profesa Lipumba na kufunguliwa kwa ukurasa mpya.

“Katiba yetu ya mwaka 1992 na toleo la mwaka 2014 haisemi chochote tofauti; anabaki kuwa mwanachama wa kawaida mwenye hadhi ya kiongozi mstaafu, ambaye tutamtumia zaidi katika kutoa ushauri,” amesema.

Katika maelezo yake, amedai kuwa Profesa mwenyewe hakuwa tayari kugombea katika uchaguzi uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024, bali alishawishiwa na baadhi ya wapambe wake kwa maslahi yao binafsi.

“Aliomba astaafu na kupisha damu changa ifanye kazi, lakini waliokuwa wanamzunguka walikuwa wanamlazimisha; ndipo alichukua uamuzi wa kugombea ili wao wanufaike kwa maslahi yao binafsi,” amesema.

Alipoulizwa kama chama kitaweza kusimama imara bila Profesa Lipumba, Shamsi amesema uimara wa uongozi hutegemea ushirikiano na wanachama, kwa kuwa wao ndio huamua mustakabali wa chama chao.

“Naamini chama kitafanya vyema, ingawa tunakabiliwa na changamoto mbalimbali kama ukosefu wa umoja, migogoro ya hapa na pale na matatizo ya kiuchumi. Haya yote yatategemea mashirikiano na wanachama wetu, kwa kuwa wao huchangia kifedha na kwa mawazo katika ujenzi wa chama chao,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *