
BEKI wa kushoto wa TRA United, Valentin Nouma, ameanza vyema maisha yake mapya ndani ya kikosi hicho, baada ya kuifungia timu hiyo bao moja na la ushindi wa 1-0, dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora, katika mechi ya Kombe la Shirikisho.
Katika mechi hiyo ya hatua ya 64 bora, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, beki huyo alicheza kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho, tangu alipojiunga nacho kwenye dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 30, 2026.
Kocha wa timu hiyo, Mrundi Etienne Ndayiragije, alisema usajili wa nyota huyo utaongeza ushindani mkubwa kwa wachezaji wenzake kutokana na uwezo wake mzuri wa kuzuia na kutengeneza mashambulizi, jambo litakaloipa faida zaidi timu hiyo.
“Ni mchezaji mzuri atakayetuongezea wigo wa machaguo katika kikosi chetu, amecheza mechi yake ya kwanza na kufunga bao moja, jambo ambalo ni nzuri kwake binafsi na kwa timu kiujumla, naamini atafanya vizuri zaidi,” alisema Ndayiragije.
Nouma alijiunga na Simba, Julai 7, 2024, akitokea FC Saint Eloi Lupopo ya DR Congo kwa mkataba wa miaka mitatu, lakini alifikia makubaliano ya kutoendelea na timu hiyo Julai 12, 2025, kutokana na kutopata nafasi ya kucheza zaidi kikosini.
Sababu za kufikia makubaliano ya pande mbili ya kusitisha mkataba na Simba, ni kutokana na kushindwa kupenya mara kwa mara mbele ya aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’, ambaye pia ameondoka na kujiunga na Yanga.
Beki huyo anatazamiwa kuongeza ushindani akiwa na TRA United, baada ya kuondoka CI Kamsar aliyojiunga nayo kwa ushawishi mkubwa wa kocha mkuu, Kamou Malo, aliyewahi kufanya naye pia kazi katika kikosi cha timu ya taifa lake la Burkina Faso.
Malo aliyekifundisha kikosi hicho cha taifa kuanzia Julai 24, 2019 hadi Februari 1, 2022, ndiye aliyempendekeza nyota huyo kusajiliwa CI Kamsar ya Guinea, huku akizichezea pia timu za Rahimo na AS Douanes zote kutoka kwao Burkina Faso.