
Francesca Albanese, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa wa maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, amesema hatajiuzulu wadhifa wake huo licha ya mashinikizo yanayotolewa dhidi yake na serikali za nchi kadhaa za Ulaya kutokana na matamshi yanayodaiwa kuwa ametoa dhidi ya utawala wa kizayuni wa Israel.
Akizungumza katika mahojiano na Euronews siku ya Ijumaa, Albanese alisema hatajiuzulu, na akazielezea tuhuma alizotoa waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa dhidi yake kwamba ameiita Israel “adui wa ubinadamu” kuwa ni za “za kipuuzi” na zinazotokana na taarifa potofu.
Mzozo huo ulianza baada ya kundi la wabunge wa Ufaransa kutuma barua kwa Jean-Noel Barrot wakimtuhumu Albanese kwa kuuelezea utawala wa kizayuni kuwa ni “adui wa ubinadamu” wakati wa mkutano wa Doha aliohutubia kwa njia ya video, wakinukuu video ambayo ilibainika kuwa ni feki.
Ujerumani, Ufaransa na Jamhuri ya Czech zimemng’ang’ania Albanese ajiuzulu kutokana na matamshi hayo. Ripota huyo maalumu wa UN amesema, utata huo ulikusudiwa kuvuruga ripoti zake zinazokosoa nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, kwa usaidizi wao wa kisiasa, kimkakati na kijeshi kwa kwa utawala wa Israel.
“Tusilifanye suala hili kuwa ni kuhusu mimi,” amesema Albanese, akielekeza kidole badala yake, kwa kile alichokiita “ripoti saba za kuapiza” zinazothibitisha uungaji mkono unaofanywa na nchi 62 kwa Israel.
Aidha amehoji, vipi kunakuwepo na ufuatiliaji mkubwa zaidi kuhusu matamshi ambayo hakutoa kuliko vitendo vinavyofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel, ambao unashutumiwa kwa kufanya uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Albanese amesisitiza kuwa ataendelea kubaki katika wadhifa wake huo kwa sababu ana kura ya imani aliyopewa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.
Zaidi ya mawaziri 150 wa zamani, wanadiplomasia na mabalozi ulimwenguni kote wameandika barua ya wazi kumuunga mkono Francesca Albanese na kumkosoa waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa kwa kusambaza taarifa potofu…/