
Ripoti za vyombo mbalimbali vya habari nchini Pakistan zinaeleza namna hali inavyozidi kuwa mbaya katika jimbo la Balochistan zikieleza kuwa serikali inasuasa kumaliza mzozo wa kisiasa unaotajwa kuwa sababu.
Inaeleza kuwa vifo, utekaji ni kati ya matukio yanayotikisa Balochistan na kutishia uhai wa wananchi na sekta mbalimbali huku wawekezaji nao wakipata hofu.
‘’Ikiwa haya yataendelea Balochistan ipo hatarini kutoka kuwa eneo salama hadi kuwa eneo la utengano na vurugu,’’
‘’Kinachoendelea Balochistan kinatishia mambo ya msingi ambayo Pakistan imeiahidi China, hata rais wa Marekani amenukuliwa akisema jeshi kutotuliza hali mbaya Balochistan ndio kichochecho cha vurugu,’’ inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Inafafanua kuwa mashambulizi yanayoratibiwa na Jeshi la Ukombozi la Baloch (BLA) na kusababisha vifo vya wananchi ndio yanayotajwa kuwa kikwazo cha biashara kati ya nchi hiyo na China, Marekani.
‘’Balochistan kuna utajiri mkubwa wa madini, vurugu zisipodhibitiwa ni wazi kuwa hali itazidi kuwa mbaya na nchi itakosa mapato,’’ inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa serikali inatakiwa kushiriki katika mazungumzo ya kisiasa kwa ajili ya kumaliza mzozo, si kudhani kinachoendelea Balochistan kinanochewa na wageni.
Usmaa Kareem ni kati ya wanahabari walioshiriki kutoa ripoti hiyo, alibainisha kuwa wakazi wa Balochistan wanadai kunyimwa uhuru wa kisiasa, ushiriki wa kiuchumi.
‘’Badala yake malalamiko yao yamepokewa kwa hisia tofauti, mitaani zinafanyika operesheni za kijeshi na watu kupotea,’’ alidai Kareem.