KATIKA mabao mawili ya Ligi Kuu aliyofunga kiungo wa Coastal Union, Cleophace Mkandala, yote ameifunga Tanzania Prisons, ambapo nyota huyo aliwahi kukitumikia kikosi hicho cha maafande, kabla ya kuondoka na kwenda kutafuta changamoto mpya.

Nyota huyo alianza kuifungia Coastal Union bao la ushindi wa 1-0, dakika ya 34, dhidi ya Tanzania Prisons, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Septemba 17, 2025, ikiwa ni ya kwanza kwa msimu huu.

Bao lake la pili pia msimu huu, akaifunga Prisons katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 4-1, ugenini kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Februari 10, 2026, alilolifunga katika dakika ya 90+4 na kuzamisha matumaini ya timu hiyo ya maafande.

Mkandala aliyezichezea Kagera Sugar, Dodoma Jiji na Azam, alifunga bao hilo, huku, Bakari Msimu akifunga mawili katika dakika ya 1, 51 na jingine likifungwa na Shiza Kichuya (dakika ya 42), wakati la Prisons lilifungwa na George Mpole (dakika ya 45).

Ushindi huo wa mabao 4-1, dhidi ya Prisons, ulikuwa ni wa kwanza kwa Coastal Union msimu huu ikiwa ugenini, kwani kabla ya hapo, ilicheza mechi sita bila kushinda, huku pia safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikishindwa kufunga hata bao.

Mechi na Prisons ilikuwa ni ya saba kwa Coastal Union kucheza ugenini msimu huu, ambapo sita zilizopita kabla ya hiyo iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikiwa haijafunga bao lolote lile.

Mabao hayo manne iliyoyapata Coastal Union dhidi ya Prisons, yalikuwa ni ya kwanza kwa kikosi hicho kuyafunga ugenini msimu huu, ambapo timu hiyo iko nafasi ya 10 kwa pointi 15, baada ya kushinda mechi tatu, sare sita na kupoteza pia sita.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkandala, alisema kufunga mabao hayo mawili kwa timu aliyowahi kuichezea ni jambo la kawaida na linalotokea mara kwa mara, ingawa suala la kushangilia au kutoshangilia linatokana na mazingira pia ya ulivyoondoka.

“Kufunga ni furaha na jambo zuri kwa mchezaji yeyote, ila suala la kushangilia inatokana na ulivyoachana pia na waajiri wako wa zamani, kwa mfano mimi niliondoka vizuri, ndio maana nilishangilia kwa ishara ya kuomba msamaha,” alisema Mkandala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *