
Mjumbe Huru wa Umoja wa Mataifa wa Kutafuta Ukweli kuhusu Sudan uliripoti mnamo Februari 19, 2026, “vitendo vya mauaji ya kimbari” huko El-Fasher, eneo linalokumbwa na ukatili baada ya kuanguka mikononi mwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) mnamo Oktoba 26, 2025.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Siku hiyo, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya “makamanda watatu wa RSF [ambao] walishiriki katika kuzingirwa kwa miezi 18 na kukamatwa kwa El-Fasher na RSF, ambapo wanamgambo hao walifanya kampeni ya kutisha ya mauaji ya kikabila, mateso, njaa, na unyanyasaji wa kijinsia.”
Wakati Umoja wa Mataifa ukizungumzia “vitendo vya mauaji ya kimbari” vilivyofanywa El-Fasher, magharibi mwa Sudan, Marekani imetangaza vikwazo vipya dhidi ya makamanda wa kijeshi walioshiriki katika mauaji katika mji huu. Mnamo mwezi Oktoba 2025, vikosi vya wanamgmbo wa Jenerali Hemedti vilishambulia mji mkuu wa Darfur Kaskazini, vikichukua udhibiti wa mji huo na kuua maelfu ya raia.
Leo, viongozi watatu kati ya hawa wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) wamewekewa vikwazo na Wizara ya Fedha ya Marekani, akiwemo mtu aliyepewa jina la utani Abu Lulu: Brigedia Jenerali El’fateh Abdullah Idris Adam, aliyepewa jina la “Mchinjaji wa El-Fasher,” kwa sababu alijirekodi akitabasamu na kuandaa mauaji ya raia wakiwa wamepiga magoti kabla ya kurusha video hizi kwenye mitandao ya kijamii.
Alikamatwa kwa muda na viongozi wakuu wa RSF ambao walikuwa wakijaribu kutuliza utata uliosababishwa na picha hizi, kabla ya kuachiliwa. Baadaye alijitokeza tena katika eneo la Kordofan, ambapo mapigano kati ya RSF ya Jenerali Hemedti na jeshi la Jenerali al-Burhan yalikuwa yakipamba moto.
Watu wengine wawili waliowekewa vikwazo hawajulikani sana: Gedo Hamdan Ahmed Mohamed na Tijani Ibrahim Moussa Mohamed, wote wakiwa makamanda wa vitengo wakati wa El-Fasher ikianguka mikononi mwa RSF.
Wote watatu wanatuhumiwa kwa mauaji ya raia na wanakabiliwa na vikwazo vya Wizara ya Fedha ya Marekani, ambavyo ni pamoja na kuzuia mali yoyote ambayo wanaweza kuwa nayo nchini Marekani na kumkataza mtu au kampuni yoyote ya Marekani kufanya biashara nao. “Tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan mnamo mwezi Aprili 2023, Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na wanamgambo washirika wametenda ukatili mkubwa, ikiwa ni pamoja na uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, na mauaji ya kimbari,” Wizara ya Fedha ya Marekani inabainisha.
Vikwazo hivi vinafuata maamuzi kama yaliyochukuliwa na Uingereza na Umoja wa Ulaya (EU), yanayowalenga watu hao.