
Dodoma. Watafiti wamebaini kuwa mkoa wa Dodoma una ardhi inayofaa kwa kilimo cha tende, baada ya majaribio ya miongo kadhaa, hali ambayo sasa inahamasisha wakulima kuchangamkia zao hili lenye soko kubwa ndani na nje ya nchi.
Sifa kuu iliyofanya Dodoma kuthibitishwa ni hali ya ukame inayofaa kwa usatwishaji wa tende, ikilinganishwa na maeneo mengine yanayokolimwa.
Utafiti wa kina umeonesha kwamba mbegu za zao hili zinaweza kustawi vizuri katika wilaya za Chamwino, Dodoma Jijini na hata Mkoa wa Singida.
Akizungumza Jumamosi, Februari 21, 2026, Dk Nicholaus Kuboja, Mratibu wa Mpango wa Kilimo cha Tende kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), amesema kwamba Dodoma sasa imejipanga kuwa na mashamba matatu ya mfano yaliyotengwa katika wilaya ya Chamwino kwa lengo la kuwafikia wakulima 250 na maofisa ugani 20.
“Tulianza mpango huu kwa ufadhili wa Serikali ya Saudi Arabia chini ya King Humanitarian Aid and Relief Centre, tukileta aina nne za mbegu ambazo zimeonyesha kustawi vizuri. Lengo ni kuhakikisha tende inakuwa chanzo cha kipato kwa wakulima na kuongeza mapato ya familia,” amesema Dk Kuboja.
Aidha, Tabu Likoko, Mtaalamu Mwelekezi kutoka Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO), amesema kila kitu kiko tayari kwa zao hili, ikiwemo mafunzo kwa maofisa ugani na miongozo ya kilimo.
“Soko la zao hili ni kubwa, gharama za kilimo ni rahisi, na tunashirikisha wakulima kuhakikisha wanachangamkia fursa hii kikamilifu,” amesema Likoko.
Mkazi wa kijiji cha Mvumi, Juma Nyheka amesema tangu utoto wake amefahamu mitende kujiotea msituni bila mpango rasmi wa kilimo.
“Hadi sasa siwezi kuamini kuna kilimo rasmi cha tende. Hata hivyo, mpango huu utasaidia wakulima kuendeleza zao hili lenye soko kubwa,” amesema Nyheka.
Kwa sasa, Mkoa wa Dodoma umejipanga kuwa kitovu cha zao la tende, ambalo linatarajiwa kuongeza mapato ya wakulima na kuchangia ukuaji wa uchumi wa vijijini na taifa kwa ujumla.