Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani
Donald Trump amewashutumu majaji sita wa Mahakama ya Juu ambao wameuwekea kizingiti
kikubwa katika muhula wake wa pili madarakani kwa kuondoa ushuru wa kimataifa
wa utawala huo.
Uamuzi wa
mahakama ya Ijumaa ulikuwa “wa kukatisha tamaa sana”. Majaji wanaoshabikia
mkumbo wa wengi wanapaswa “kujitafakari” kwani wamekosa ujasiri wa “kufanya jambo sahihi”, Trump alisema, katika majibu yake yaliyogeuka kuwa mashambulizi makubwa
dhidi ya mhimili huru wa serikali iliyo na haki sawa.
Uamuzi huo ulikuwa ushindi mkubwa kwa wafanyabiashara na mataifa ya Marekani ambayo yamepinga majukumu hayo, na kufungua mlango kwa uwezekano wa kurejeshewa ushuru wa mabilioni ya dola, huku pia ikizua msukosuko mpya katika mazingira ya biashara ya kimataifa.
Kujibu amuzi wa Mahakama hiyo hata hivyo Rais Donald Trump ameweka ushuru mpya wa asilimia 10 wa kimataifa kuchukua nafasi ya zile zilizotupiliwa mbali na Mahakama ya Juu, akiitaja uamuzi huo kuwa “mbaya” na kuwakashifu majaji waliokataa sera yake ya biashara kama “wajinga”.
Rais alizindua mpango huo muda mfupi baada ya majaji kuharamisha ushuru mwingi wa kimataifa ambao Ikulu ya White House ilitangaza mwaka jana.
Alipozindua ushuru huu uliotupiliwa mbali na mahakama Aprili iliyopita alisema “nchi yetu na walipakodi wake wameibiwa kwa zaidi ya miaka 50”. Akihoji kwamba Marekani inanunua bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi kuliko inazouza, fedha za Wamarekani zinatumika nje ya nchini bila sababu za msingi.