Neema akiwa mbele ya kibanda anakoishi, nyuma yake kuna mtoto anayetazama kamera wakati picha inapigwa.

Muda wa kusoma: Dakika 3

“Mvua inaponyesha, tunalowa kama kuku. Maisha tunayoishi hapa ni mabaya sana. Chawa walioko kwenye nguo zetu wanatufanya tuugue kutokana na ukosefu wa usafi. Bado tumevaa nguo zile zile ambazo tulikuwa tumevaa tukiondoka nyumbani kwetu”

Neema Amos ambaye anaishi katika kambi ya wakimbizi ya Cishemere eneo la Cibitoke, Nchini Burundi, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anatusimulia jinsi hali ilivyo.

Neema anaishi katika nyumba moja ndogo iliyojengwa na nyasi kwa sababu hakufanikiwa kupata hema katika kambi hiyo. Anaishi na watoti wake watano, na Jirani yake ambaye alimsaidia kukimbia nyumbani kwao eneo la Luvungi, nchini DR-Congo.

Katika kambi ya Cishmere, raia 8,500 wa DRC wanaishi pale wakitarajia kuhamishwa na kupelekwa kwa kambi zenye mazingira bora za Busuma eneo la Ruyigi.

Burunditayari ilikuwa ni nyumbani kwa zaidi ya wakimbizi 70,000 wa DRC, kabla ya wakimbizi wengine 70,000 kuwasili baada ya 90,000 kukimbia vita mwezi Disemba mwaka uliopita haswa kutoka maeneo ya Uvira na Luvungi.

Kambi ya Cishemere, imezingirwa na ua, na wakimbizi hawaruhusiwi kutoka ila wanaweza kaa karibu na lango kuu la kambi hiyo.

Ndani ya kambi hiyo nyumba zimejengwa na tofali, nyasi, wengi wanaishi kwa mabanda na hema,wengine waliokosa makazi walijijengea nyumba za matope.

Mvua inayonyesha kipindi hiki imefanya hali kuwa mbaya zaidi kwa wakimbizi wanoishi hapa .

Watoto,watu wazima pamoja na wazee ndani ya kambi hiyo hukaa kwa makundi wakitarajia yeyote atakaye zuru kambi hiyo kuwafaa na misaada.

Faida Bizizi mwenye umri wa miaka 65, alikimbia kutoka eneo la Lubarika, aliiambia BBC kuwa ‘Nimeona mengi katika maisha yangu, ila vita vilivyofanya nikimbilie huku vilikuwa vibaya mno. Nilikimbia nikiwa nimebeba wanangu, nikihepa vizuizi njiani, bado nakumbuka. Nimekuwa hapa tangu tarehe 15 mwezi Disemba mwaka uliopita.”

Faida Bizizi anasema siku ya kwanza walipofika katika kambi ya Cishemere, “tulipewa mchele na maharagwe (mara moja kwa siku, na chakula hicho kinapatikana saa saba wala saa nane”. Ila (mambo imebadilika, hivi wanapewa ugali na maharagwe mara moja kwa siku.

Tatizo kubwa wanalokumbana nalo wakimbizi hawa ni kwamba watoto hawawezi kwenda shule kwa sababu hakuna shule katika kambi. Baadhi yao wanaishi kwa kuomba omba.

Freddy Kassim Kashindi, mwenye umri wa miaka 24, anasema kuwa wanaishi katika banda moja lililojengwa kuishi watu 60, ila wanalala ndani zaidi ya watu 100. “Mvua ikinyesha tunalala tukiwa tumesimama”

Irène Roza, msichana wa umri wa miaka 17, ambaye kwa sasa haendi shuleni anatuelezea kuwa “sisi wasischana tunaishi Maisha magumu. Tunakula mara moja kwa siku na sio chakula kizuri. Kipindi cha hedhi huwa kigumu kwasababu hatuna sodo, Maisha ni magumu”

Hadja Lahbib akizungumza na watoto waliokimbia makazi yao katika kambi ya Cishemere.

Wakimbizi bado wanahofia kurejea makwao nchini DRC, kwa sababu hawaamini kuwa amani ipo au itarajea tena kutokana na mapigano yanayoshuhudiwa mara kwa mara.

Siku ya Jumatano, wakimbizi kutoka kambi ya Cishemere walitembelewa na Hadja Lahbib, kamishna mkuu wa umoja wa Ulaya anayesimamia misaada ya kibinadamu katika ziara yake ya kuzuru DRC, Burundi na Rwanda.

Hadja Lahbib, akiwa katika kambi hiyo alitoa wito kwa wanaopigana mashariki mwa DRC kuheshimu mkataba wa kusitisha vita. “Tuwape afueni wale wote ambao wamekuwa wakikimbia vita Maisha yao yote.”

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuharirwa na Prime Ndikumagenge

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *