Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Yasmin Rufo
- Nafasi, BBC News
-
Muda wa kusoma: Dakika 4
Kuanzia kutosa uso kwenye maji ya barafu, hadi kutumia vifaa vya barafu na kuzipitisha kwenye mashavu, mitandao ya kijamii imekuwa ikielezea mbinu tofauti za kupunguza uvimbe wa uso kwa muda mfupi.
Ingawa mbinu hizi zinaushawishi, daktari wa ngozi wanasema mbinu hizo zinatafsiriwa vibaya, zinashabikiwa kupita kiasi na ni za muda mfupi.
Dkt wa Ngozi Aiza Jamil anasema uvimbe wa uso unatokana na mwili kuhifadhi maji kupita kiasi,na hii hutokana na kutumia chumvi kupita kiasi,unywaji pombe na ukosefu wa usingizi.
Dkt Tina Tian ambaye pia ni daktari wa ngozi, anaelezea kuwa mbinu za kupunguza uvimbe wa uso zimegawanyika mara tatu, kutumia barafu, kukanda uso na kujaribu kukaza uso.
“Zinaweza kupunguza uvimbe kwa kiwango kikubwa na kutoa nafuu ya muda mfupi, ila haiwezi badilisha muonekano wa uso.”
Ila mbinu ipi haswa inafaa kutumika kupunguza uvimbe wa uso?
hizi hapa ni njia tatu ambazo zinaweza kutumika;
kutumia maji baridi/barafu
Chanzo cha picha, Getty Images
Kama ushawahi kufikiria kutumbukiza uso wako kwenye beseni la barafu hauko pekee yako.
Kuosha uso kutumia barafu imekua mbinu inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kama mbinu ya kudumisha urembo na pia kufunza mwili kuwa na uwezo wa kustahimili.
Tina anaelezea kuwa mbinu hiyo inatokana na kuwa “baridi hufanya mishipa ya damu kubana na kupunguza uvimbe”
Hii ndio mantiki ya kutumia barafu kukanda uso na kutumia kinyago kilichowekwa kweny jokofu.
Tina anasema hauhitaji kujitumbukiza kwenye barafu nyingi ili kupata matokeo, kwani kukanda uso na barafu au kuosha na maji baridi bado hukupa matokeo mazuri.
Aiza anaongezea kuwa inaweza “kukaza uso wako, kufanya uso wako kuwa na upya fulani asubuhi” ila matokeo haya ni ya muda mfupi, “hudumu kwa masaa kadhaa wala sio siku kadhaa” anasema.
Tina anasema kuwa kuna tofauti kati ya kupata muonekano mzuri na kufanya kwa kupitiliza. “Matumizi ya barafu kwa wingi kunaweza kuharibu ngozi yako au kusababisha ugonjwa wa ngozi wa rosacea, kwa hivyo ni bora kufanya kwa uangalifu.”
Rola za uso
Chanzo cha picha, Getty Images
Zamani rola zilikuwa zikitumiwa na watu wachache katika spa maalum, lakini sasa rola za uso na mawe ya gua sha zimekuwa vifaa vya kawaida bafuni mwa wengi.
Zinatangazwa kama vifaa vya kubadilisha muonekano wa uso, zimejijengea sifa ya kuunda umbo la uso, lakini Aiza anasema “hazikazi ngozi kwa muda mrefu, hazibadilishi muundo wa ngozi, wala haziondoi mafuta.”
Anaongeza kuwa ni bora kuziona kama “vifaa vya kutuliza.”
Hata hivyo, zinaweza kusaidia kupunguza uvimbe wa uso kwa muda.
“Ukandaji wa uso husaidia kupunguza mkusanyiko wa maji usoni ikiwa zitatumiwa mara kwa mara,” Tina anasema.
Unapoziviringisha au kuzipitisha juu ya ngozi, inasaidia maji yaliyotuama kusonga na kupunguza uvimbe.
Tina anaongeza kuwa kugandisha vifaa hivyo kunaweza kuboresha matokeo, ndiyo maana baadhi ya watu huzihifadhi kwenye jokofu.Tina anahoji kuwa vifaa hivyo vinafaa kutumiwa kwa upole na uangalifu ili kuzuia michubuko.
Krimu za Kafeini
Chanzo cha picha, Getty Images
Natumai umeona mafuta ya uso yaliyotengenezwa na kahawa au Kafeini, na imekuwa ikipendekezwa na watengeneza maudhui kwenye mitandao ya kijamii, na wengi wao huitumia sana sana majira ya asubuhi ili kupata macho yaliyongaa.
Ngozi karibu na macho hupata uvimbe kwa haraka kwa sababu maji yanaweza kujikusanya hapo.
Tofauti na mitindo mingine ya urembo, Tina anasema hili lina ushahidi wa kufanya kazi.
“Kafeini hupunguza upana wa mishipa hivyo krimu za macho zenye kafeini zinaweza kwa kweli kupunguza uvimbe” anasema
Kafeini hubana mishipa ya damu kwa muda, na kupunguza upana wa mishipa na baadaye kupunguza uvimbe unaonekana usoni. Aiza anaongeza kuwa inaweza kusaidia “kupunguza mkusanyiko wa maji mwilini na baadhi ya weusi chini ya macho.”
Ikiwa utatumia krimu ya macho, Tina anapendekeza utafute iliyo na viambato vya kulainisha na kuhifadhi unyevunyevu pamoja na kafeini, kwa kuwa hilo husaidia kuboresha ngozi.
Anaongeza kuwa unaweza pia kuihifadhi krimu hiyo kwenye jokofu au hata “kuipaka kwa kutumia kijiko baridi”
Aiza anasema kuwa kutumia kijiko baridi au mifuko ya chai iliyowekwa kwenye jokofu ” hupunguza uvimbe kwa muda na kutuliza ngozi.”
Ingawa krimu ya macho yenye kafeini inaweza kusaidia kupunguza uvimbe, Tina anasema ni muhimu zaidi kuzingatia chanzo cha tatizo.
“Punguza matumizi ya chumvi kwa wingi na pombe, pata usingizi wa kutosha na lala kama umeinua kichwa chako kidogo”
Uvimbe mwingi si tatizo la kiafya na hupungua wenyewe, lakini Tina anasema kuwa “ikiwa unaendelea kwa muda mrefu, unaongezeka, unauma au unaambatana na dalili nyingine kama matatizo ya kupumua ni vyema kumwona daktari.”
Imetfasiriwa na Beldeen Waliaula