
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Jose Manuel Albares amesema, ilikuwa ni “makosa” kwa Kamishna wa Umoja wa Ulaya kuhudhuria mkutano wa uzinduzi wa ‘Bodi ya Amani’ ya Rais wa Marekani Donald Trump mjini Washington.
Albares ametoa kauli hiyo katika hafla iliyofanyika mjini Barcelona, baada ya Trump kuitisha mkutano wa kundi lake jipya siku ya Alkhamisi, na kuwaleta pamoja wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 20 kwa lengo lililotajwa kuwa ni kujadili ujenzi mpya wa Ukanda wa Ghaza na kufanya juhudi pana za utulivu na uthabiti kimataifa.
Japokuwa Umoja wa Ulaya, EU umekataa kujiunga na bodi hiyo ya Trump, lakini ulimtuma Kamishna wa kanda ya Mediterania Dubravka Suica kuhudhuria sehemu moja ya mkutano huo iliyohusiana na Ghaza.
“Iliniuma kumuona kamishna wa Umoja wa Ulaya ambaye hangepaswa kuwepo huko,” ameeleza waziri wa mambo ya nje wa Uhispania.
Huku akieleza kuwa, anaheshimu kile alichokiita “juhudi” za Trump, amesisitiza kwamba “kuna njia zingine” za kuweza kuifikia amani katika Mashariki ya Kati.
Albares ameeleza bayana kwamba Umoja wa Ulaya unaunga mkono suluhisho la mataifa mawili kwa mzozo wa Palestina na kwa hivyo “hauwezi kushiriki” katika shirika lolote linaloitenga Mamlaka ya Taifa ya Palestina.
Aidha, amesema serikali ya Uhispania ilikataa mwaliko wa kushiriki kwa sababu Wapalestina hawakujumuishwa na kwamba mpango wa amani uliobuniwa na Marekani “unaibua mashaka makubwa kuhusu utangamano wake na sheria za kimataifa”…/