Mambo yameendelea kuwa magumu kwa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele licha ya timu yake Pyramids FC kuibuka na ushindi wa bao 1-0 jana kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Misri dhidi ya Ceramica Cleopatra.

Wakati Pyramids FC ikifurahia ushindi huo ambao umeifanya ifikishe pointi 34 na kujikita katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Misri, Mayele ameondoka kichwa chini kwa kushindwa kupachika bao katika mechi hiyo.

Kwa kushindwa kufunga jana, Mayele sasa amefikisha idadi ya michezo 21 mfululizo ya mashindano tofauti ambayo amecheza bila kufunga bao.

Tangu alipofunga mara ya mwisho, Oktoba 21 mwaka jana katika mchezo dhidi ya Pharco, Mayele hajafumania nyavu tena katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Katika michezo hiyo 21 mfululizo ambayo Mayele hajafunga bao, mechi 15 ni za mashindano ya Klabu na michezo iliyobaki sita ni ya timu ya taifa.

Ukame huo wa Mayele unakuja katika kipindi ambacho mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31, mkataba wake na Pyramids FC unaelekea ukingoni ambapo utafikia tamati Juni 30, 2026.

Ikiwa hali hiyo itaendelea hivyo, inaweza kutibua ndoto za Mayele kujiunga na Ligi Kuu ya Saudi Arabia ambayo alikaribia kufanya hivyo katika uhamisho wa dirisha kubwa mwaka jana.

Mayele alihitajika na Al Ittifaq inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia lakini Pyramids FC iligoma kumuachia Mfungaji huyo Bora wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Msimu uliopita ulionekana kuwa mzuri kwa Mayele baada ya kuibuka kinara wa kufumania nyavu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akipachika mabao sita.

Mabao hayo sita yalitoa mchango mkubwa katika kuiwezesha Pyramids FC kutwaa taji la mashindano hayo ikifanya hivyo kwa mara ya kwanza.

Mayele siku chache baadaye aliiongoza Pyramids FC kutwaa ubingwa wa mashindano ya FIFA ya klabu za Asia, Afrika na Oceania baada ya kuifungia mabao matatu.

Mayele tangu alipojiunga na Pyramids FC, Julai 30, 2023 akitokea Yanga, ameifungia timu hiyo ya Misri mabao 49 katika michezo 112.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *