Mwanza. Serikali inatarajia kufunga na kusambaza mifumo ya umeme wa jua katika visiwa 65 vya mkoani Mwanza kwa bei ya ruzuku, mradi utakaogharimu zaidi ya Sh4.8 bilioni.

Akizungumza katika kisiwa cha Bezi leo Jumamosi, Februari 21, 2026 wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Jones Olutu amesema kati ya fedha hizo, Serikali imelipia Sh3.3 bilioni huku Sh1.5 bilioni zilizobaki zikitarajiwa kulipwa na wananchi watakaounganishiwa huduma hiyo.

Olutu amesema kwa kuanzia, mifumo hiyo itafungwa katika kaya 200 katika kisiwa cha Bezi, hatua itakayofanya jumla ya kaya 500 kupata umeme huo baada ya kaya 300 kuunganishiwa katika awamu ya kwanza.

Amesema katika kisiwa hicho kuna kaya na vibanda vya biashara 600, ambapo mwekezaji Power Gen tayari aliunganisha kaya 300 na kubaki kaya na vibanda 300 vikiwa havijafikiwa.

“Katika kisiwa cha Bezi kuna wananchi wengi wenye uhitaji wa umeme. Kupitia mradi huu kaya nyingine 200 zitaunganishiwa na kufanya jumla ya kaya 500 kunufaika,” amesema.

Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati, Salome Makamba akimkabidhi mkazi wa Kisiwa cha Bezi Sola Paneli wakati wa uzinduzi wa mradi wa ufungaji umeme jua maeneo ya visiwani kwa bei ya ruzuku utakaofikia visiwa 65 vya Mkoa wa Mwanza.

Ameongeza kuwa pamoja na Bezi, mifumo hiyo itasambazwa katika visiwa vya Tafu na Ukara ambavyo navyo vitapata umeme wa jua kwa bei ya ruzuku.

Olutu amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 wananchi wote wanapata huduma ya umeme na kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Meja Jenerali (mstaafu) Jacob Kingu amesema bodi itaendelea kusimamia rasilimali za REA kwa uwajibikaji ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora na kuwafikia walengwa.

Amesema katika kipindi cha 2021 hadi 2026, vijiji 12,318 vimefikiwa na huduma ya umeme, hali iliyochangia kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme nchini.

Akizindua mradi huo, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema upatikanaji wa umeme katika kisiwa cha Bezi utarahisisha shughuli za uvuvi na kuongeza kipato kwa wananchi.

Amesema mkandarasi anatakiwa kuongeza kasi ili kukamilisha mradi huo ifikapo Mei 2027 kama ilivyopangwa.

“Hatutaongeza muda kwa mkandarasi. Afanye kazi kwa weledi na kwa wakati ili wananchi waone matokeo ya dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwafikishia huduma ya umeme,” amesema.

Makamba pia ameiagiza REA pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha mifumo inayofungwa inakuwa salama na endelevu.

Kwa upande wake, Edson Gabo akitoa salamu za Wizara ya Nishati amesema sekta ya nishati imeendelea kuimarika, ambapo hadi sasa gridi ya Taifa inazalisha zaidi ya megawati 4,000.

Mkazi wa Bezi, Mageni Francis amesema umeme huo utaondoa gharama za mafuta ya jenereta na kuongeza ari ya wafanyabiashara wa samaki kununua majokofu kwa ajili ya kuhifadhi mazao ya samaki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *