Unguja. Ukuaji wa sekta ya viwanda Zanzibar umeshuka kutoka asilimia 8.4 katika robo ya tatu ya mwaka 2024 hadi asilimia 2.7 katika robo ya tatu ya mwaka 2025, hali inayochangia kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa visiwa hivyo.

Ripoti ya mwelekeo wa Mpango wa Taifa na Bajeti ya Serikali 2026/27 inaonyesha kuwa uchumi wa Zanzibar ulikua kwa asilimia 7.0 kati ya Julai na Septemba 2025, ikilinganishwa na asilimia 7.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2024.

Moja ya sababu zilizotajwa ni kushuka kwa ukuaji wa sekta ya viwanda hadi asilimia 2.3 kutoka asilimia 5.7 mwaka uliotangulia.

Akiwasilisha ripoti hiyo katika kikao cha pili cha Mkutano wa 11 wa Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil amesema kupungua kwa uzalishaji viwandani ndiko kumeshusha kasi ya sekta hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imekutana na wadau wa sekta binafsi kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kuinua sekta hiyo, ambayo ni muhimu katika kukuza ajira na uchumi.

Taifa limeweka lengo la kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2030.

Mwenyekiti wa Baraza la Viwanda na Uzalishaji Zanzibar (MCZ), Ahmed Yussuf Baalawy amesema changamoto kubwa ni ukosefu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali, huku akisisitiza kuwa bila utekelezaji wa makusudi, mikutano haitaleta matokeo.

Amesema viwanda vinahitaji kulindwa ili bidhaa za ndani zipate soko la uhakika.

“Bila kulinda viwanda vyetu haviwezi kukua. Serikali ni mnunuzi mkubwa, lakini mara nyingi inaagiza bidhaa kutoka nje badala ya kununua zinazozalishwa hapa,” alisema.

Baalawy pia amegusia suala la kodi ya ongezeko la thamani (VAT), akisema utekelezaji wake hauko sawa kwa wadau wote, jambo linaloongeza mzigo kwa wazalishaji wa ndani.

Mkurugenzi Mkuu wa Inaya Zanzibar Ltd, Cheherazade Cheikh, amesema utitiri wa kodi na tozo ni mwiba mkubwa kwa wazalishaji.

Naye Meneja Uhusiano wa Kiwanda cha Sukari Zanzibar, Beatrice Millinga, ameeleza kuwa kuna pengo kubwa la mawasiliano kati ya taasisi za Serikali na sekta binafsi.

Kwa upande wake, Meneja wa Kiwanda cha Maji cha Drop Zanzibar, Mahamoud Hassan Bakar, amesema ukosefu wa umeme wa uhakika ni kikwazo kikubwa kwa uzalishaji.

“Umeme ukikatika kwa saa tano, unategemea uzalishe nini? Tunahitaji umeme imara ili tuweze kushindana,” amesema.

Ameongeza kuwa bila mpango kazi madhubuti, viwanda vitaendelea kudorora na kusababisha kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

Pia, amelalamikia tozo nyingi kutoka taasisi mbalimbali bila uratibu wa pamoja.

Mdau mwingine, Hussein Meena, amependekeza kuwepo kwa leseni moja jumuishi badala ya wazalishaji kuhitajika kupata vibali kutoka taasisi nyingi.

Aidha, ameeleza kuwa bidhaa za Zanzibar hukumbana na vikwazo zinapotaka kuingia soko la Tanzania Bara au nje ya nchi.

Katibu wa Zanzibar Exporters Association (Zexa), Khamis Issa Mohammed, amesema kodi na tozo ni kubwa kuliko mapato ya baadhi ya wazalishaji, hali inayokatisha tamaa wawekezaji.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Dk Habiba Hassan Omar, amesema Serikali inatambua changamoto hizo na inaandaa mkakati wa kuanzisha maeneo maalumu ya viwanda ili kurahisisha huduma za miundombinu, kodi na tozo.

Amesema baadhi ya changamoto kama umeme na bandari ni za kitaifa na zinaendelea kushughulikiwa, huku akiahidi kuwa Serikali itaweka mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya viwanda ili ichangie zaidi katika ukuaji wa uchumi na ajira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *