Kundi moja la wabeba silaha limewaua watu wasiopungua 50 na kuwateka nyara wanawake na watoto katika shambulio la usiku kwenye kijiji kimoja kilichoko kaskazini magharibi mwa Jimbo la Zamfara nchini Nigeria.

Kwa mujibu wa wananchi na mamlaka husika, shambulio hilo lilianza Alkhamisi usiku na kuendelea hadi jana asubuhi katika kijiji cha Tungan Dutse kilichoko kwenye eneo la Bukkuyum jimboni Zamfara, wakati watu waliobeba silaha walipofika hapo wakiwa wamepanda pikipiki na kuanza kuyachoma moto majengo na kuwateka nyara raia.

“Wamekuwa wakitoka kijiji kimoja na kuelekea kingine … na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 50,” ameeleza Hamisu A Faru, mbunge anayewakilisha eneo la Bukkuyum Kusini.

Faru amevieleza vyombo vya habari kwa njia ya simu kwamba idadi ya watu waliotekwa nyara bado haijajulikana kwa sababu maafisa wa eneo hilo wangali wanakusanya orodha ya waliotoweka.

Wakazi wamesema ishara za onyo zilionekana kabla ya shambulio hilo.

Abdullahi Sani, mkazi wa hapo mwenye umri wa miaka 41, amesema wanakijiji waliviarifu vikosi vya usalama baada ya kuona zaidi ya pikipiki 150 zikiwa zimebeba watu wenye silaha siku moja mapema, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.

“Hakuna mtu aliyelala jana; sote tuna maumivu,” ameeleza Sani na kuongeza kwamba wanafamilia wake watatu waliuawa katika shambulio hilo.

Maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Nigeria yanaendelea kukabiliana na vitisho vya usalama vinavyoandamana, ikiwa ni pamoja na magenge ya wahalifu wenye silaha na wapiganaji wa makundi ya waasi…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *