
Kahama. Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mwaka huu 2026, unatarajiwa kufanyika wilayani Kahama mkoani Shinyanga kwa siku mbili, Februari 27 na 28, huku wadau zaidi ya 600 wakitarajiwa kuhudhuria.
Uwepo wa mkutano huo, unatarajiwa kuibua fursa mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu wilayani humo, pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali.
Akizungumza na wanahabari leo Februari 21, 2026, wilayani Kahama, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, Azan Mufti, amesema ujio wa mkutano huo ni heshima kubwa kwa wakazi wa Kahama na kanda ya ziwa kwa ujumla.
Amesema mkutano huo utatoa nafasi kwa wadau wa soka kujadili changamoto na kuweka mikakati mipya ya kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu Kahama ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa utakaokuwa na uwezo wa kupokea mashabiki zaidi ya 7,000.
“Mkutano huu utatoa nafasi kwa wadau wa soka kujadili changamoto na kuweka mikakati mipya ya kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu Kahama, ukiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa utakaokuwa na uwezo wa kupokea mashabiki zaidi ya 7,000 kwa wakati mmoja,” amesema Mufti.
Mufti amesema Rais wa TFF, Wallace Karia atawasili wilayani humo Februari 25, 2026, kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuelekea mkutano huo.
Awali mkutano huo ulipangwa kufanyika Februari 21, 2026, wilayani Kahama, kabla ya kusogezwa mbele hadi Februari 27 na 28, 2026.
Hafidh Alawi ni mdau wa soka Kahama, amesema ni vyema viongozi waliopo ngazi ya wilaya wakatumia fursa ya uwepo wa mkutano huo kuibua na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo kwenye soka la Kahama.
“Ujio wa huu mkutano, viongozi wetu wautumie kutafuta wapi penye changamoto za soka letu Kahama ili tupiga hatua. Uwanja ni mbovu, miaka yote tunaambiwa unajengwa na haukamiliki, wasipige tu makofi watumie fursa vizuri,” amesema mdau huyo.
Naye Samuel John, dereva bodaboda Kahama, amesema ujio wa mkutano huo ni fursa kwa wafanyabiashara, na kuwasihi kuwa waaminifu ili kutengeneza taswira nzuri na fursa zaidi katika wilaya hiyo.
“Wafanyabiashara tunachotakiwa kufanya ni kuwa waaminifu kwa sababu ujio wa mkutano huu ni fursa kubwa kwetu tukiutumia vyema, pia utavuta fursa nyingine zaidi kwenye mji wetu,” amesema.