Serengeti. Asilimia 24 ya wanafunzi waliotakiwa kuripoti kwa ajili ya kuanza elimu ya kidato cha kwanza katikaHalmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kwa mwaka huu bado hawajaripoti shuleni hadi sasa.

Jumla ya wanafunzi 5,250 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari za Serikali katika halmashauri hiyo ambapo hadi sasa ni wanafunzi 3,975 ndio walioripoti shuleni

Takwimu hizo zimetolewa mjini Mugumu wilayani Serengeti leo Jumapili Februari 22,2026 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Tumsifu Mushi kwenye hafla ya kukabidhi mahitaji ya shule kwa watoto wanaotoka katika mazingira magumu, msaada uliotolewa na taasisi ya Nyansaho.

Amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya elimu ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kupata elimu hivyo ni vema jamii kwa ujumla ikashirikiana na Serikali ili kufikia malengo hayo.

“Miundombinu inaendelea kuboreshwa, elimu pia inatolewa bila malipo kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita lakini wazazi wanatakiwa kununua mahitaji maalumu kwa ajili ya watoto kusoma, niwaombe wana jamii kwa ujumla tuhakikishe hili linafanikiwa,” amesema

Mushi amefafanua kuwa ili kufanikisha lengo hilo tayari suala hilo la chakula cha mchana kwa wanafunzi limefanywa kuwa ajenda ya kudumu kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji na kata ili wazazi waweze kushiriki kikamilifu kwa kutoa chakula katika shule hizo.

Amesema tayari msako umeanza kuwatafuta wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni ambapo amesema uongozi wa wilaya hiyo unatarajia kuwa na idadi ya angalau asilimia 90 ya wanafunzi waliochaguliwa wawe wameripoti shuleni.

“Tunataka kuwaona shuleni angalau kwa asilimia 90 wakiwa kwenye shule zetu na hizo asilimia 10 watakuwa ni wale waliokwenda shule binafsi hivyo niwaombe wananchi kila mwenye mwanafunzi ahakikishe mtoto wake anakwenda shule,”amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Serengeti, Mary Daniel amesema ofisi yake kwa kushirikiana na taasisi hiyo wametumia zaidi ya Sh60 milioni ili kufanikisha upatikanaji wa mahitaji hayo ya wanafunzi hasa wanaotoka katika mazingira magumu.

Amesema jumla ya wanafunzi 361 wa kidato cha kwanza kutoka katika kaya maskini ambao walikuwa hawana mahitaji ya shule wamenufaika na msaada huo ambao umehusisha sare za shule, daftari kalamu na mahitaji mengine.

Ametoa wito kwa wazazi kuendelea kuwapeleka watoto wao shuleni hata kama hawana mahitaji muhimu kwani Serikali imewaagiza walimu kuwapokea wanafunzi wote hata kama hawana mahitaji.

Baadhi ya watoto wanaotoka katika mazingira magumu wakisubiri kupokea msaada wa mahitaji ya shule kutoka Taasisi ya Nyansaho wilayani Serengeti.  Picha na Beldina Nyakeke

Amesema suala la elimu kwa watoto ni la muhimu kwani bila elimu hakuna maendeleo na kwamba Serengeti iliyo bora zaidi inapatikana kwa watu wake kupata fursa ya kusoma.

Mratibu wa Taasisi ya Nyansaho, Modesta Mwema amesema mbali na kutoa msaada huo, taasisi hiyo pia itahakikisha inawafuatilia wanufaika wote ili watoto hao waweze kuendelea na masomo yao.

“Hakuna haja ya mtoto kushindwa kwenda shule kwa sababu ya kutoka mazingira magumu, wadau tuungane wote watoto waweze kusoma,” amesema

Baadhi ya wakazi wa Serengeti wamesema zipo sababu kadhaa zinawafanya wazazi washindwe kuwapeleka shule watoto wao ikiwepo suala la uelewa mdogo kuhusu elimu.

“Kuna baadhi ya wazazi hawaoni sababu ya mtoto kuendelea na elimu pale anapohitimu darasa la saba hivyo wanaanza kuwashirikisha katika shughuli za uzalishaji mali kama kilimo,” amesema Mogenka Msamba

Msamba amesema ili kukomesha tabia hiyo ni vema hatua kali zikachukuliwa dhidi ya wazazi wanaokatisha ndoto za elimu kwa watoto wao ili iwe fundisho kwa wengine.

Ghati Nyakiboha ameomba ufadhili huo uwe endelevu ili watoto hao waweze kusoma hadi kuhitimu kidato cha nne kwa maelezo kuwa wazazi wa watoto hao hawana uwezo wa kumudu mahitaji ya shule.

“Tuliambiwa watoto kama hawana mahitaji muhimu wao waende tu lakini nilijiuliza ataenda hivyo hadi lini kwani sikuwa na namna yoyote ya kupata pesa ili nimnunulie mahitaji hayo,” amesema Mwita Mosongo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *