Chanzo cha picha, Reuters
-
- Author, Edited by Stephen Hawkes and Andrew Webb
- Nafasi, BBC World Service
-
Muda wa kusoma: Dakika 8
Andrew Mountbatten-Windsor amekamatwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma.
Kukamatwa huku kunakuja siku ambayo mkuu huyo wa zamani anatimiza umri wa miaka 66.
Alikamatwa Sandringham, huko Norfolk, ambapo amekuwa akiishi tangu alipoamriwa kuondoka katika jumba lake la kifahari la Windsor, Royal Lodge.
Maafisa wanaendelea kupekua mali zote mbili.
Mkuu huyo wa zamani amekabiliwa na madai mengi kuhusu uhusiano wake na mnyanyasaji wa kingono wa watoto aliyehukumiwa Jeffrey Epstein, lakini kukamatwa kwake hakuhusiani na mashtaka ya makosa ya kingono.
Hii inakuja baada ya Polisi wa Thames Valley kusema walikuwa wakitathmini malalamiko kuhusu madai ya kutoa nyaraka za siri kwa mkuu huyo wa zamani, alipokuwa mjumbe wa biashara, na Epstein.
Andrew Mountbatten-Windsor hapo awali alikana kosa lolote kuhusiana na Epstein; hajajibu maombi ya BBC ya kutoa maoni kuhusu madai hayo maalum kuhusiana na kutolewa kwa mamilioni ya faili za Epstein mnamo Januari 2026.
Mfalme Charles III alisema “alisikitishwa” na kukamatwa kwa Andrew, akiongeza “sheria lazima ichukue mkondo wake”.
Jeffrey Epstein alikuwa nani na alikuwa na mahusiano yapi na Andrew?
Epstein alikuwa meneja wa mifuko ya uwekezaji ambaye alifariki mwaka wa 2019 akiwa gerezani akikabiliwa na mashtaka ya biashara haramu ya ngono na kula njama. Mchunguzi wa matibabu wa New York alithibitisha kifo chake.
Mnamo 2005, wazazi wa mtoto wa miaka 14 waliwaambia polisi wa Florida kwamba Epstein alikuwa amemnyanyasa binti yao nyumbani kwake Palm Beach. Utafutaji wa polisi ulipata picha za wasichana kote nyumbani.
Epstein alihukumiwa kifungo cha miezi 18 jela na kuachiliwa kwa muda wa majaribio baada ya miaka 13.
Mnamo Julai 2019, Epstein alikamatwa New York, baada ya kurudi kutoka Paris kwa ndege yake binafsi.
Mnamo Agosti, alikutwa amekufa katika seli yake katika Kituo cha Magereza cha Metropolitan cha New York, ambapo alikuwa akisubiri kesi yake.
Epstein alishtakiwa kwa kuwalipa wasichana walio chini ya umri wa miaka 18 kufanya vitendo vya ngono katika majumba yake ya kifahari ya Manhattan na Florida kati ya 2002 na 2005.
Alikana kosa lolote na alikana mashtaka dhidi yake.
Chanzo cha picha, News Syndication
Andrew alikiambia kipindi cha Newsnight cha BBC, mnamo 2019, kwamba alikuwa amekata mawasiliano yote na rafiki yake wa zamani mnamo Desemba 2010, baada ya kukutana katika Hifadhi Kuu ya New York.
Lakini barua pepe zimeibuka zikionesha Andrew aliwasiliana na Epstein faraghani miezi kadhaa baadaye, huku akiahidi “kukutana naye tena hivi karibuni”.
Maelezo mapya pia yaliibuka kuhusu urafiki wa mke wa zamani wa Andrew, Sarah Ferguson, na Epstein.
Shirika la hisani la Ferguson, Sarah’s Trust, lilitangaza kwamba litafungwa “kwa mustakabali unaoonekana” baada ya barua pepe kuonekana kuonesha kwamba alikuwa akiwasiliana na Epstein alipokuwa gerezani kwa kuomba ngono kutoka kwa mtoto mdogo.
Ilikuwa Prince Andrew akawa Bw. Windsor?
Chanzo cha picha, Getty Images
Mfalme Charles III alimvua ndugu yake Prince Andrew cheo chake cha kifalme cha “Mwana Mfalme” mwezi Oktoba 2025.
Wakati huo, Buckingham Palace ilisema kwamba “mawazo na pole za dhati za Mfalme zimekuwa, na zitaendelea kuwa, pamoja na waathiriwa na manusura wa aina zote za unyanyasaji.”
Andrew aliacha vyeo vyake vingine vya kifalme, ikiwa ni pamoja na Duke of York, mapema mwezi Oktoba 2025, baada ya tawasifu ya Virginia Giuffre iliyochapishwa baada ya kifo chake, Nobody’s Girl, kurudia madai kwamba alimnyanyasa kingono mara tatu tofauti alipokuwa bado kijana. Andrew amekuwa akikanusha madai hayo kila mara.
Ikijibu taarifa ya Ikulu, familia ya Bi Giuffre ilisema kwamba “alimwangusha mwana wa mfalme wa Uingereza kwa ukweli wake na ujasiri wake wa ajabu.” Bi Giuffre alijiua mapema mwaka huu.
Andrew anaishi wapi?

Mnamo 2003, Andrew alisaini mkataba wa kukodisha Royal Lodge – jumba la kifahari lenye vyumba 30, lililoorodheshwa Daraja la II huko Windsor Great Park, karibu na Kasri la Windsor.
Mnamo Februari 2026, alihamia makazi binafsi yaliyofadhiliwa na Mfalme Charles III katika Sandringham Estate.
Kwanini Prince Andrew bado yuko kwenye orodha warithi wa kiti cha enzi
Prince Andrew bado ni wa nane katika urithi wa kiti cha enzi, akifuatiwa na binti zake, Princess Beatrice ambaye ni wa tisa, na Princess Eugenie ambaye ni wa 12.
Mwongozo kutoka Maktaba ya House of Commons unaonesha kuwa hali hiyo inaweza kubadilishwa, hata hivyo, kupitia sheria ya Bunge.
Kuna mfano wa awali. Sheria ya mwaka 1701 ilisababisha Prince Michael of Kent kuondolewa katika orodha ya urithi wa kiti cha enzi alipooa Mkatoliki mwaka 1978, ingawa alirejeshwa tena miaka 37 baadaye, baada ya kupitishwa kwa sheria mpya ya urithi wa taji, na sasa yuko katika nafasi ya 53 kwenye mstari wa urithi.
Lakini kumwondoa Andrew pia kutahitaji idhini ya nchi nyingine zote 14 ambazo Mfalme Charles anatawala:
- Antigua and Barbuda
- Australia
- The Bahamas
- Belize
- Canada
- Grenada
- Jamaica
- New Zealand
- Papua New Guinea
- Saint Kitts and Nevis
- Saint Lucia
- Saint Vincent and the Grenadines
- Visiwa vya Solomon
- Tuvalu
Virginia Giuffre alikuwa na shutuma gani dhidi ya Andrew?
Chanzo cha picha, US Department of Justice
Katika kesi ya kiraia ya Marekani ya mwaka 2021, Bi. Giuffre alimshtaki Andrew kwa kumnyanyasa kingono.
Katika hati za mahakama, alisema alikuwa mwathiriwa wa biashara haramu ya ngono na unyanyasaji wa kingono na mfadhili Jeffrey Epstein tangu akiwa na umri wa miaka 16 na hii ilikuwa ni pamoja na “kupelekwa” kwa wanaume wengine wenye nguvu kama vile Andrew, ambao walimnyanyasa kingono mara tatu tofauti kabla ya kutimiza miaka 18.
Chanzo cha picha, Mark Harrison / BBC
Prince Andrew amekuwa akikanusha kwa uthabiti madai ya Virginia Giuffre dhidi yake na akaambia Newsnight kwamba hakumbuki kamwe kukutana naye.
Pande zote mbili zilikubaliana kufikia makubaliano nje ya mahakama mwaka 2022, ambapo Andrew alimlipa Virginia Giuffre kiasi kisichofahamika, bila kutambua uwajibikaji.
Kitabu cha Virginia Giuffre kinaeleza nini ?
Virginia Giuffre alihofia kwamba atakufa akiwa “mtumwa wa ngono” mikononi mwa Jeffrey Epstein na marafiki zake, inavyoonyesha katika tawasifu yake iliyochapishwa baada ya kifo chake, Nobody’s Girl.
Pia, katikati ya unyanyasaji huo alikuwa mpenzi wa zamani wa Epstein, Ghislaine Maxwell, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa usafirishaji wa watoto kwa ajili ya ngono.
Miaka mingi baadaye, Virginia Giuffre anakumbuka jinsi alivyokuwa akiwahofia wote wawili. Na sehemu kubwa ya kitabu hicho ni ya kusoma kwa huzuni kubwa, huku akielezea unyanyasaji wa kikatili wa Epstein, ambao ulimpelekea “maumivu makubwa.
Kitabu cha Virginia Giuffre kinaeleza nini kuhusu Andrew?
Mnamo Machi 2001, Maxwell inadaiwa alimuamsha na kumwambia kwamba ni “siku maalum” na “kama Cinderella” atakutana na “mwana wa kifalme mwenye mvuto,” anaandika Virginia Giuffre.
Walipokutana, anakumbuka kwamba Maxwell alimtaka Prince Andrew, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 41, kubashiri umri wake.
Alibashiri “sahihi, 17,” anaongeza Virginia Giuffre, akisema: “Binti zangu [Princess Beatrice na Princess Eugenie] ni wachanga kidogo kuliko wewe.”
Usiku huo, yeye, Jeffrey Epstein na Ghislaine Maxwell walikwenda kwenye klabu ya Tramp mjini London pamoja na Prince Andrew, ambaye “alitetemeka” Virginia Giuffrenaliandika.
Kisha, wakiwa wanasafiri kurudi kwenye nyumba ya Maxwell, Maxwell inadaiwa kumwambia: “Tutakaporudi nyumbani, utamfanyia kile unachomfanyia Jeffrey.”
“Alikuwa rafiki kiasi, lakini bado alikuwa na hisia za kana kwamba aliamini kuwa na ngono nami ilikuwa haki yake ya kuzaliwa,” anaandika Virginia Giuffre.
“Asubuhi iliyofuata, ilikuwa wazi kuwa Maxwell alikuwa ameshawasiliana na rafiki yake wa kifalme kwa sababu alimwambia, ‘Umefanya vizuri. Mwana wa kifalme alifurahia.'”
Chanzo cha picha, US Department of Justice / PA Media
Virginia Giuffre, kwa upande wake, “hakujihisi vizuri sana,” anaandika, akiongeza: “Hivi karibuni, Epstein ataniongezea $15,000 kwa kumtumikia mtu ambaye magazeti yalimuita ‘Randy Andy’, pesa nyingi.”
TakribanI mwezi mmoja baadaye, anasema, alifanya ngono na Prince Andrew kwa mara ya pili, katika townhouse ya Epstein mjini New York.
Tukio la tatu linalodaiwa lilitokea katika kisiwa cha Jeffrey Epstein, kama sehemu ya kile ambacho Virginia Giuffre anaelezea kama “orgy,” yaani hali ambapo watu wengi hushiriki katika tendo la ngono pamoja wakati mmoja.
“Epstein, Andy na takriban wasichana wengine wanane pamoja nami tulifanya ngono pamoja,” anasema.
“Wasichana wengine wote walionekana kuwa chini ya umri wa miaka 18 na hawakuongea Kiingereza kweli.”
“Epstein alicheka kuhusu jinsi walivyokuwa hawawezi kuwasiliana vizuri, akisema kuwa wao ndio wasichana rahisi zaidi kushirikiana nao.”
Chanzo cha picha, Getty Images
Akirejelea makubaliano ya nje ya mahakama ya mwaka 2022, Virginia Giuffre anaandika: “Nilikubali amri ya kimya kwa mwaka mmoja, ambayo ilionekana muhimu kwa mwana wa kifalme kwa sababu ilihakikisha sherehe ya Platinum Jubilee ya mama yake haingeharibiwa zaidi ya ilivyokuwa tayari.”
Chanzo cha Buckingham Palace kiliambia BBC kuwa maafisa wa kifalme walikubali kuwa kuchapishwa kwa kitabu hicho kunaweza kumaanisha “siku zaidi za maumivu yajayo”.
Ni mambo gani mengine polisi wa Uingereza wanachunguza?
Polisi wa Jiji la London “wanachunguza kwa makini” ripoti ya gazeti ambapo Andrew alimwomba afisa aliyepewa jukumu la kuwa mlinzi kumpekua kutazama chochote kinachomhusisha na Bi Giuffre mnamo 2011.
Ripoti hiyo, katika gazeti la Mail on Sunday, ilisema Andrew alimpa mlinzi huyo tarehe yake ya kuzaliwa na nambari ya Usalama wa Jamii ya Marekani ili kujaribu kufichua kama alikuwa na rekodi ya uhalifu au taarifa nyingine yoyote inayoweza kumharibia.
Wakati huo, vyanzo vya kifalme vilisema shutuma hii dhidi ya Andrew ilikuwa ikitendewa kwa “wasiwasi mkubwa sana na inapaswa kuchunguzwa kwa njia zinazofaa kwa kiwango kamili”.
Andrew aliacha kuwa mtumishi wa kifalme mnamo 2019.
Chanzo cha picha, Getty Images
Ni mambo gani mengine yamechangia kuanguka kwa Prince Andrew?
Nyaraka za siri zinazofichua uhusiano wa Andrew na jasusi anayedaiwa kuwa wa China zilifichuliwa Aprili 2025, baada ya BBC na vyombo vingine vya habari kusukuma mahakama kuwaachilia huru.
Zinafichua jinsi Andrew alivyoamini angeweza kuokoa nafasi maarufu ya umma kwa kutafuta fursa za biashara nchini China kwa msaada wa mfanyabiashara wa Kichina Yang Tengbo, ambaye mshauri wake wa zamani Dominic Hampshire alimchukulia Andrew kama “mwanga pekee mwishoni mwa handaki” baada ya mahojiano yake ya Newsnight ya 2019.
Nyaraka hizo pia zinafichua maelezo ya “njia ya mawasiliano” ya Andrew na Rais wa China, Xi Jinping, ambayo ilijumuisha kutuma barua ya kuzaliwa ya kila mwaka, na jinsi huduma ya usalama ya Uingereza, MI5, ilivyoingilia kati kuonya dhidi ya mawasiliano yoyote na Bw. Yang.
Chanzo cha picha, Getty Images
Taarifa ya ushahidi ya Bw Hampshire pia inaonyesha kwamba:
- Uhusiano wa Prince Andrew na Bw Yang ulijadiliwa katika mikutano miwili kati ya Bw Hampshire na Mfalme Charles III, ambapo Andrew aliingizwa kwa siri katika Windsor Castle ili kuepuka vyombo vya habari.
- Mvutano miongoni mwa wasaidizi wa Andrew ulisababisha katibu wake binafsi kuondolewa katika baadhi ya mikutano kuhusu mipango yake ya biashara.
Andrew alisema alikuwa “amekata mawasiliano yote” na Bw Yang baada ya kupokea ushauri kutoka serikalini. Alisema mikutano yote ilikuwa “kupitia njia rasmi”, na kwamba “hakuna jambo nyeti lililowahi kujadiliwa”.
Bw Yang alisema maelezo yaliyomwita jasusi yalikuwa “si ya kweli kabisa”.