KIUNGO mshambuliaji wa Mashujaa, Seleman Rashid ‘Bwenzi’, anakaribia kufikisha mwaka mzima bila ya kufunga bao lolote la Ligi Kuu, tangu mara ya mwisho nyota huyo alipofunga wakati akiwa na kikosi cha KenGold cha jijini Mbeya, Februari 27, 2025.

Nyota huyo aliyejiunga na Mashujaa, Agosti 12, 2025, baada ya KenGold kushuka daraja kutoka Ligi Kuu hadi Championship, mara ya mwisho kufunga ilikuwa sare ya bao 1-1, dhidi ya maafande wa JKT Tanzania Februari 27, 2025.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, Dar es Salaam, Bwenzi alifunga bao hilo la kusawazisha dk85, baada ya mshambuliaji, Edward Songo kuifungia JKT kwa penalti dk45+6.

Bao hilo ni la mwisho kwa Bwenzi katika Ligi Kuu, ambapo nyota huyo anakaribia kufikisha mwaka mzima, huku msimu huu akiwa na kikosi hicho cha maafande wa Mashujaa, amechangia moja tu dhidi ya JKT Tanzania.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, Bwenzi aliasisti bao la Mundhir Vuai dk78, baada ya Paul Peter, kuisawazishia JKT dk86 na pambano hilo la maafande kuisha sare ya 1-1, Septemba 18, 2025.

Akizungumzia kiwango chake msimu huu, Bwenzi, alikiri kupitia changamoto hiyo ingawa sababu kubwa ni ushindani wa nafasi na nyota wenzake kikosini humo, japo ataendelea kupambana zaidi ili kurudisha imani kwa mashabiki wake.

“Ni upepo mbaya tu ambao mchezaji yeyote anapitia, kwangu naichukulia changamoto kwa sababu mwanzoni nilivyotarajia na sasa kiukweli ni tofauti, naamini nitarudi katika kiwango kizuri na mashabiki wangu wataanza kufurahia,” amesema Bwenzi.

Kabla ya kujiunga na KenGold, katika dirisha dogo la Januari 2025, alikuwa Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship msimu huu, na 2024-2025, alifunga bao moja na kuasisti mawili.

Akiwa na KenGold kwa msimu wa 2024-2025, alichangia mabao sita ya Ligi Kuu, baada ya kufunga matano na kuasisti moja tu, akishika nafasi ya pili kwa kuchangia mengi kikosini, nyuma ya Mishamo Michael, aliyefunga matano na kuasisti mawili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *