Arusha. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, ametaka uongozi wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (AIST-NM) kukamilisha ujenzi wa bweni kwa wakati ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Amesema hayo leo Jumapili, Februari 22, 2026, wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika ujenzi wa bweni la wanafunzi wa ngazi ya uzamili na uzamivu katika fani za sayansi, teknolojia na ubunifu, mkoani Arusha.

Dk Mwigulu amefika mkoani Arusha kuanza ziara za kukagua na kuweka mawe ya msingi ya miradi mbalimbali ya maendeleo, akitokea mkoani Kilimanjaro na Tanga, alikofanya kazi hizo.

“Taarifa nilizopewa zinaonesha ujenzi wa jengo la bweni umezingatia ubora unaohitajika. Ujenzi huu ni ushahidi wa dhamira njema ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuthamini elimu kama nyenzo muhimu ya kufikia maendeleo ya kweli,” amesema Dk Mwigulu.

Waziri Mkuu, Dk.Mwigulu Nchemba (kushoto) akimsikiliza Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Profesa Maulilio Kipanyula wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la Bweni la wanafunzi wilayani Arumeru mkoani Arusha leo. Picha na Filbert Rweyemamu

Amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye elimu kwa kutambua umuhimu wa matumizi sahihi ya teknolojia kama njia inayoharakisha kazi na kuongeza tija.

Amesema ameona kwenye maonesho ya ubunifu namna teknolojia inavyoweza kukausha tumbaku kwa kutumia nishati ya jua na kupunguza matumizi ya kuni.

Waziri Mkuu amesema, katika kutambua umuhimu huo, kila mkoa nchini una taasisi ya elimu ya ngazi ya kati na juu, na Serikali imeongezeka bajeti ya elimu ya juu kutoka Sh464 bilioni hadi zaidi ya Sh 900 bilioni, na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na fedha za kujikimu.

Aidha, Dk Mwigulu amesema juhudi za Serikali za kuwekeza fedha nyingi kwenye taasisi za elimu zinalenga kuwajengea uwezo Watanzania kuwa na maarifa yatakayoweza kushindana kwenye soko la ajira duniani.

Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema taasisi hiyo ni ya kipekee, na Serikali inakitegemea kitumike kutoa wanasayansi bora watakaotatua changamoto katika jamii.

“Mheshimiwa Rais wetu ameagiza uwekezaji kwenye sayansi na teknolojia, na kila mkoa una shule ya sekondari ya wasichana, lengo likiwa kuongeza idadi ya wanasayansi. Pia, tumewawezesha vijana kusoma nje ya nchi kwenye vyuo vikuu vinavyoheshimika duniani,” amesema Profesa Mkenda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la AIST-NM, Balozi Maimuna Tarish, amesema taasisi hiyo imeongeza ubunifu na kuiwezesha kuongoza kwa watafiti wake kazi zao kupewa hati miliki kutoka serikalini.

Waziri Mkuu, Dk.Mwigulu Nchemba (mwenye skafu) akiongozwa na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akikagua Bweni la wanafunzi katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi ya Nelson Mandela. Picha na Filbert Rweyemamu

Amesema kati ya maombi yanayowasilishwa Brela ya hati miliki, asilimia 54 yanatoka taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.

Balozi Tarish amesema mradi huo wa mabweni, hadi utakapokamilika, utagharimu Sh7.9 bilioni na unalenga kuongeza udahili kwa wanafunzi wanaolala chuoni kutoka 279 hadi 459 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM), Joshua Nassari, ameomba Serikali kujenga barabara mbadala ili kuendana na mazingira ya sasa, badala ya kutegemea barabara moja pekee inayotoka Moshi kuingia Arusha.

Amesema kuwepo kwa barabara ya mchepuko ni suala la kiusalama na litafungua mkoa wa Arusha kupitika pindi kunapotokea dharura kwenye barabara kuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *