
MSHAMBULIAJI wa Kagera Sugar, Hassan Mwaterema, amesema siri ya mwenendo mzuri kwa kikosi hicho hadi sasa katika Ligi ya Championship msimu huu, ni kutokana na ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wao, jambo linalowapa motisha ya kupambana.
Nyota huyo alirejea tena Kagera Sugar, Agosti 23, 2025, baada ya mkataba wake na Dodoma Jiji aliyojiunga nayo Julai 5, 2022, akitokea katika kikosi hicho cha ‘Wanankurukumbi’ kuisha, ambapo hadi sasa amekuwa na kiwango kizuri akiwa na timu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwaterema amesema malengo yake makubwa ya kwanza ni kuhakikisha timu hiyo inarejea tena Ligi Kuu Bara, baada ya kushuka daraja msimu wa 2024-2025, ilipomaliza katika nafasi ya 15, ikikusanya pointi 23.
“Malengo yangu mengine ni kuibuka pia mfungaji bora, ila jambo hilo silipi kipaumbele sana kwa sababu nataka kuona timu inarejea Ligi Kuu, ubora wa washindani wetu unatupa hamasa sisi wachezaji ya kuzidi kupambana zaidi,” amesema Mwaterema.
Nyota huyo anakumbukwa msimu wa 2017-2018, alipoibuka mfungaji bora wa Ligi ya Championship baada ya kufunga mabao 16, akiwa na kikosi cha maafande wa JKT Tanzania, ambapo kwa msimu huu hadi sasa tayari ameifungia Kagera Sugar mabao saba.
Kagera iliyodumu Ligi Kuu kwa miaka 20, tangu iliposhiriki mwaka 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, ikiwa nafasi ya 15 kwa pointi 23, japo msimu huu wa 2025-2026, iko nafasi ya pili kwa pointi 43, nyuma ya vinara, Geita Gold yenye 46.