Shirika la Amnest International limelaani mashambulizi ya Marekani katika eneo la Karibiani na huko Pasifiki.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetaja mashambulizi ya Marekani dhidi ya meli zinazoshukiwa kusafirisha madawa ya kulevya katika bahari ya Karibiani na Pasifiki, ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 140 kuwa ni kinyume cha sheria.

Ujumbe uliotumwa katika akaunti rasmi ya  Amnesty International katika mtandao wa kijamii wa X na kwenye tovuti yake rasmi kufuatia ripoti ya jeshi la Marekani kuhusu kuharibiwa meli tatu na kuuawa takriban watu 11 katika maji ya Karibiani na Pasifiki umeeleza kwamba: Mashambulizi hayo yaliyotekelezwa ndani na nje ya Venezuela hayana msingi wowote wa kisheria, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ambayo kulingana na ripoti, yamesababisha vifo vya raia kadhaa. Amnesty International imeyataja mashambulizi hayo ya Marekani kuwa tishio kwa usalama wa kikanda na yaliyokiuka mamlaka ya kitaifa ya kujitawala nchi za maeneo ya pwani ambayo yanapasa kukomeshwa. 

Shirika la Amnesty International limetahadharisha kuwa hatua mtawalia na zisizodhibitiwa za kijeshi za Marekani zinaweza kusababisha vifo na majeruhi wengi na kujiri ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Shirika hilo lisilo la kiserikali limelitaka Bunge la Marekani kufuatilia suala hili ili kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa na wahusika wote wa mashambulizi hayo wanawajibishwa.

Shirika hili la haki za binadamu pia limesisitiza kuhusu ulazima wa kuchukuliwa hatua na kufanyika uchunguzi huru; na kutaka kuundwa tume isiyoegemea upande wowote ya kuchunguza kikamilifu matukio hayo na kufuatika kesi za manusura na familia za wahanga. 

Hii ni katika hali ambayo Marekani imesalia kimya mkabala wa watu waliouawa, na kutotoa ripoti ya wazi kuhusu sababu ya mashambulizi hayo kumeathiri imani ya ulimwengu mkabala wa madai yake  kuhusu haki za binadamu. Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani imehalallisha mauaji hayo kwa kudai kuwa inaendesha vita dhidi ya “magaidi wa madawa ya kulevya” huko Amerika ya Latini hata hivyo hadi sasa haijatoa ushahidi wowote wenye mashiko kwamba meli inazozishambulia zinajihusiha na magendo ya madawa ya kulevya; jambo lililoibua mjadala mkubwa kuhusu uhalali wa oparesheni za kijeshi za Marekani. 

Marekani imefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya meli katika visiwa vya Karibiani tangu mwanzoni mwa mwezi Septemba 2025 kwa kisingizio cha kupambana na biashara ya madawa za kulevya, na hadi sasa watu wasiopungua 140 wamepoteza maisha kutokana na mashambulizi ya Marekani. 

Karibu mwezi mmoja uliopita, familia mbili huko Trinidad na Tobago ziliwasilisha kesi yao ya kwanza katika mahakama za Marekani dhidi ya serikali yaTrump kuhusu vifo vya watu wawili katika familia hizo waliouawa katika mashambulizi ya Marekani dhidi ya boti zilizoshukiwa kuwa zinasafirisha mihadarati  huko Karibiani Oktoba 14, mwaka jana.

Wataalamu wa sheria za kimataifa na makundi ya haki za binadamu wanamini kuwa mashambulizi hayo ni mauaji ya kiholela kwa sababu yamewalenga raia ambao si tishio la papo kwa hapo kwa Marekani.

Wakati huo huo Amnsety International imewasilisha sababu kadhaa za msimamo wake wa ukosoaji, ikinukuu kanuni za msingi za sheria za kimataifa.

Sababu ya kwanza ya kulaani mashambulizi ya Marekani, ni kutokana na kukiukwa wazi haki ya kuishi na kukiukwa sheria za kimataifa za haki za binadamu. Amnesty International imesisitiza kuwa matumizi mabaya ya nguvu ya wanajeshi wa Marekani katika operesheni hizi tajwa  yanakinzana wazi na kanuni za uwiano na udharura wa kijeshi. Kwa mujibu wa ripoti za awali, aghalabu ya boti zilizoshambuliwa hazikuwa za kijeshi bali zilikuwa tu boti za uvuvi au meli ndogo za kibiashara ambazo zilishambuliwa kimakosa au bila kutolewa tahadhari za kutosha. Mauaji ya raia au watu ambao hawakuwa tishio la moja kwa moja kwa maisha ya wanajeshi wa Marekani ni ukiukaji wa wazi wa haki ya kuishi; mauaji ambayo hayawezi kuhalalishwa kwa hali yoyote ile. 

Mbali na hili, Amnesty International imeashiria kukosekana uwazi katika katika taratibu za kisheria. Shirika hilo limebainisha kuwa oparesheni za kijasusi na kijeshi za Marekani katika maeneo ya Karibiani na Pasifiki hazikuwa na usimamizi huru wa vyombo vya sheria. Wanajeshi wa Marekani katika matukio mengi, walikuwa wakishambulia moja kwa moja na kuharibu boti za wavuvi na za wafanya biashara badala ya kuwatia mbaroni na kuwafikisha katika vyombo vya sheria washukiwa. Kukosekana hatua za kuzuia za kutoa tadhadhari, kusimamisha vyombo vya baharini na kufyatua risasi moja kwa moja kwa lengo la kuua, kunaakisi sera inayopuuza haki za msingi za binadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *