Takribani watu 50 wameuawa na wanawake pamoja na watoto kadhaa kutekwa nyara katika shambulio la kigaidi lililolenga kijiji kimoja katika jimbo la Zamfara, kaskazini-magharibi mwa Nigeria.

Mashambulizi hayo, yaliyotekelezwa na magaidi  yalianza usiku wa Alhamisi na kuendelea hadi asubuhi ya Ijumaa. Washambuliaji waliwasili wakiwa juu ya pikipiki, wakachoma moto majengo na kuwapiga risasi wakazi wa kijiji cha Tungan Dutse waliokuwa wakijaribu kukimbia.

Mbunge wa jimbo hilo, Hamisu Faru, alithibitisha tukio hilo akisema: “Hakuna aliyelala tangu Alhamisi, hadi asubuhi ya leo. Baadhi ya watu wamepoteza wanafamilia watatu.”

Miili ya waathiriwa imezikwa katika mazishi ya pamoja, ikiwa imevikwa sanda nyeupe siku ya Jumamosi. Idadi kamili ya waliotekwa bado haijabainika, huku maafisa wa eneo hilo wakiendelea kuhesabu waliopotea.

Hali ya usalama nchini Nigeria inaendelea kuwa mbaya, hususan katika ukanda wa kaskazini-magharibi ambako Zamfara ipo. Eneo hilo limekumbwa kwa muda mrefu na mashambulizi ya makundi ya uhalifu, utekaji nyara na mauaji, hali iliyopelekea maelfu ya watu kuyahama makazi yao na wengine wengi kubaki katika mazingira hatarishi.

Serikali ya Nigeria imechukua hatua kadhaa kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo kupeleka wanajeshi na kushirikiana na washirika wa kimataifa kama Marekani katika msaada wa kiufundi na ubadilishanaji wa taarifa za kijasusi. Hata hivyo, changamoto zinaendelea kutokana na mwingiliano wa vitisho vya kiusalama vinavyotokana na magenge yenye silaha na makundi ya waasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *