Canada. Kuna wakati ndoa huonekana kama daraja la kuvuka kwenda kesho iliyo bora. 

Lakini yapo pia mazingira ambayo ndoa hugeuka mtego ikawa ndoana inayomnasa aliyeitega. 

Hili ndilo lililompata Aja Mali (28) (si jina halisi), kijana wa asili ya Kihindi aliyeingia Marekani kwa mkataba wa kazi wa muda mfupi.

Aja alikuwa mfanyakazi mzuri. Tatizo lake halikuwa utendaji, bali muda. Alijua fika kuwa kibali chake cha kuishi na kufanya kazi kingeisha pamoja na mkataba wake. 

Badala ya kujiandaa kurejea nyumbani au kutafuta njia halali ya kuendelea kubaki, alichagua mkato yaani mpango wa ndoa.

Kwa kutumia ujana wake na maneno matamu, Aja alijenga uhusiano na Linnie (60) (si jina halisi), mwanamke tajiri mwenye nyumba na akiba ya kutosha. Tofauti ya umri ilikuwa kubwa, lakini kwa Aja hilo halikuwa kikwazo. Lengo lilikuwa moja: kupata udhamini wa kudumu wa kuishi “majuu”.

Mapenzi yao yalionekana kushika kasi. Ndoa ikafungwa. Linnie akaongeza jina la mumewe kwenye akaunti ya benki, akaanza mchakato wa kumdhamini ili apate kibali cha kudumu cha kuishi nchini humo. Wapo waliotazama ndoa hiyo kwa jicho la mashaka—ndugu, marafiki na majirani. 

Wengine waliona Aja ameifuata fedha; wengine wakihisi Linnie naye alitaka kutumia ujana wa Aja kujiridhisha kihisia na kimwili. Kimsingi, kila mmoja alikuwa na lake moyoni.

Kadri mchakato wa udhamini ulivyokaribia kukamilika, nyufa zikaanza kuonekana. Aja alianza kuhamisha fedha kwenda kwenye akaunti yake binafsi. Simu zikawa nyingi, mazungumzo marefu kwa lugha ya kwao, mara nyingi nje ya chumba cha kulala. Ukaribu ukapungua. Mapenzi yakageuka maigizo.

Linnie alihisi mabadiliko, lakini akajipa moyo. Hadi siku Aja alipomwambia wazi kuwa mara tu udhamini utakapokamilika, angeondoka nyumbani kwake. Hilo lilikuwa pigo zito kwa mwanamke aliyewekeza hisia, heshima na mali zake katika ndoa hiyo.

Badala ya kulia au kuomba, Linnie aliamua kujibu kivyake. Akiwa tayari ana tatizo la kukosa usingizi na amepewa vidonge na daktari, alitumia mazingira hayo kupanga kisasi cha kutisha.

Siku moja alimwandalia mumewe chakula kama kawaida lakini akachanganya vidonge vya usingizi kwa wingi.

Aja alikula bila shaka. Usingizi mzito ukamvaa. Alipojilaza, Linnie alichukua mto na kumziba hewa hadi akafariki. Baadaye, kwa msaada wa binti yake, mwili ukatupwa eneo la viwanda jirani. Ndoa ikageuka jinai. Mpango wa kumtumia mwenzake ukaishia kuwa mtego wa mauti.

Kisa hiki, japokuwa cha kusisimua na cha kuhuzunisha, kinabeba funzo zito. Ndoa si chombo cha kufanikisha mipango fiche. Pale inapojengwa juu ya hila, tamaa au matumizi ya upande mmoja, huzaa maafa. 

Wote wawili katika simulizi hii waliingia wakiwa na ajenda—mmoja akitaka uraia, mwingine akitaka ujana na mapenzi. Mwishowe, tamaa na hila vikameza wote.

Ndoa ni taasisi ya uaminifu, si mkakati wa kuhalalisha maslahi binafsi. Inapogeuzwa kuwa ndoana ya kunasa fursa, siku moja ndoana hiyo humrudia aliyeitega.

Yapo mengi ya kujifunza katika simulizi kama hizi. Lakini somo kuu ni hili: usiingie kwenye ndoa ukiwa na mpango wa kumtumia mwenzako. 

Maana wakati mwingine, mchezo wa karata tatu huisha kwa kilio na gharama yake huwa kubwa kuliko faida iliyotarajiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *