
Nilitendwa na mwanaume niliyempenda na niliamini tungeoana kwa maneno mazuri aliyokuwa akiniambia, lakini hilo halikutimia akamuoa rafiki yangu wa karibu.
Kuna kijana kwa miezi kadhaa sasa amekuwa anisumbua kutaka tuzungumze akidai nikimkubalia anapeleka posa kwetu kwa ajili ya ndoa na ahitaji chochote kutoka kwangu hadi tutakapofunga ndoa. Ila naogopa naona yatatokea ya mwanzo nifanyeje?
Pole sana kwa kuogopa yaliyokukuta. Kweli vijana wa mjini wanasema wasiwasi ndiyo akili, lakini wahenga waliwahi kusema mavi ya kale hayanuki. Hivyo usihofie kuanza upya kwa sababu ya mambo yaliyotokea siku zilizopita. Maisha lazima yaendelee.
Watu na tabia zao hazifanani kila mtu ana tabia zake na kila uhusiano unahitaji msingi wa heshima, kuaminiana, na malengo sawa. Hivyo, yaliyotokea siku za nyuma yasiathiri unachotaka kukifanya sasa. Jipe muda wa kutafakari bila kufuatisha kijana anakuambia maneno matamu kiasi gani, fikiria, upe nafasi moyo kuamua bila kuingiza yaliyotokea kwa mpenzi wa kwanza.
Si vibaya pia ukiangalia tabia za kijana anayetangaza kukuoa. Mwanaume mzuri kwa ndoa ni yule anayeonyesha heshima, kuaminiana, na uwajibikaji bila shinikizo au kuhitaji chochote kutoka kwako isipokuwa mahusiano yenu. Angalia kama anathibitisha maneno yake kwa vitendo je, anakuonyesha heshima kwa familia yako, anaendelea kukuunga mkono bila masharti, na je, ana maono sawa na yako kwa maisha ya ndoa? Hii ni muhimu kwani wanaume wote hawafanani, na kutathmini tabia yake kutakusaidia kuona kama anaweza kuwa mwenzi bora kwako.
Hakikisha kijana huyo anafahamu kuwa uhusiano wa kimapenzi au kuzungumza kwa karibu hauhusiani na kutoa chochote cha haraka au ahadi zisizo na msingi. Hii inakusaidia kudumisha heshima yako binafsi na kuhakikisha kwamba maamuzi yako yanatokana na kutaka kweli, si kutokana na shinikizo au hofu ya kupoteza mpenzi. Una haki ya kusema hapana kwa hofu yoyote au presha yoyote.
Tafakari kwa kina kuhusu hisia zako na matarajio yako ya maisha. Fikiria uhusiano unaoweza kudumu, sio tu furaha ya muda mfupi. Angalia kama kijana huyu ana sifa zinazokufaa ikiwamo maadili, na uwezo wa kushirikiana nawe katika kila hali ya maisha.
Jaribu kuzungumza naye kwa muda, kumuelewa vyema, na kuona jinsi anavyoshughulika na migongano, changamoto, na maamuzi madogo ya kila siku. Kwa kufanya hivi, utaona kama anafaa kwa ndoa. Maana kuna wakati unakutana na kijana anavutia lakini ukizungumza naye hata kujenga hoja ni changamoto. Huyu mkikwaruzana au likitokea jambo linahitaji busara kulitatua atakupa shida maana atakuwa haelewi anataka nini. Huu ni mfano tu, si kwamba akishindwa hilo atashindwa na mengine.
Nakukumbusha tu huwezi kuishi bila mwenza, hivyo yaliyopita si ndwele jipange kuganga yajayo. Kinachoangaliwa kwa mwanaume ni upendo ni uwajibikaji kwa maana ya mwanaume anayejimudu ambaye atatimiza majukumu ya familia badala ya kuwa mzigo anayehitaji kuhudumiwa.
Kamwe usianze kujitwisha majukumu ya kugharamia mnapotokea kwa ajili ya matembezi, kununua zawadi za gharama kubwa, kumpa pesa, huyo atakuwa mumeo hayo utamfanyia lakini kwanza asimamie majukumu yake kama mume na kichwa cha familia, usimzoweshe kuhudumiwa atakuja kukusumbua baadaye.