
Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Madhama Kardinali Polycarp Pengo, akimtaja kama mchungaji mwaminifu aliyejitoa kwa dhati kulitumikia Kanisa na Taifa.
Salamu hizo zimewasilishwa kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, akionesha masikitiko yake Baba Mtakatifu na mshikamano wake na waumini wa Tanzania katika kipindi hiki cha majonzi.
Katika ujumbe wake, Papa Leo XIV amesema Kanisa limepoteza kiongozi mwenye busara, aliyesimama imara katika kulinda na kufundisha imani, huku akionesha unyenyekevu na moyo wa huduma kwa watu wa rika zote. “Tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na utumishi wa Kardinali Pengo, aliyetoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Kanisa na malezi ya watumishi wake,” sehemu ya ujumbe huo imenukuliwa.
Huduma ya Kiaskofu na malezi ya makleri
Baba Mtakatifu amekumbusha kwa namna ya pekee mchango wa Kardinali Pengo katika malezi akieleza kuwa juhudi zake zimeacha alama isiyofutika katika historia ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam na majimbo mengine aliyoyahudumia nchini.
Kwa zaidi ya miongo kadhaa ya utumishi wa Kiaskofu, Kardinali Pengo alihudumu katika majimbo mbalimbali ya Tanzania, akijipambanua kwa msimamo thabiti wa mafundisho ya Kanisa na juhudi za kuimarisha taasisi za kichungaji, elimu na huduma za kijamii.
Uongozi wa Bara la Afrika
Papa Leo XIV pia amesisitiza mchango wa Pengo katika ngazi ya kimataifa, hususan alipohudumu kama Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar (SECAM).
Kupitia nafasi hiyo, Kardinali Pengo alichangia kuimarisha mshikamano wa Maaskofu wa Afrika na kukuza sauti ya Kanisa la Bara hilo katika mijadala ya kijamii, kiimani na kimaadili.
“Aliunganisha Maaskofu wa Afrika kwa moyo wa undugu na maono ya pamoja,” umeeleza ujumbe wa Papa, ukimtaja Kardinali Pengo kama daraja la umoja na mshikamano.
Kanisa na Taifa linaomboleza
Kifo cha Kardinali Pengo kimeacha pengo kubwa siyo tu kwa waumini wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam bali pia kwa Kanisa la Tanzania na Afrika kwa ujumla. Viongozi wa dini, Serikali na waumini wa kada mbalimbali wameendelea kumiminika kutoa salamu za pole na kutambua mchango wake katika kuimarisha maadili, amani na mshikamano wa kijamii.
Kwa salamu zake, Papa Leo XIV amehitimisha kwa kuwaombea waumini wote wanaoomboleza, akimkabidhi marehemu katika huruma na upendo wa Mungu, akitumaini apokee thawabu ya watumishi waaminifu katika uzima wa milele.
Kwa namna alivyotumikia kwa uadilifu na uthabiti, jina la Kardinali Polycarp Pengo litaendelea kukumbukwa kama alama ya uongozi wa kiroho uliotukuka katika historia ya Kanisa Katoliki Tanzania.