
Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limelaani hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Morocco dhidi ya mashabiki 18 wa Senegal waliopatikana na hatia ya kufanya vurugu kufuatia fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON.
Rais wa kamati ya mawasiliano ya FSF, Bacary Cisse, amesema uamuzi huo umeleta mshangao na huzuni kubwa.
“Tumesikitika na kushangazwa sana na hukumu hiyo,” alinukuliwa akisema. “Uamuzi huu usioeleweka umeibua hasira kali.”
Cisse amesema matukio ya vurugu hutokea katika viwanja mbalimbali duniani, ikiwa ni pamoja na Morocco, bila kupelekea adhabu kama hizo.
“Hatua iliyochukuliwa dhidi ya mashabiki hawa yanaoonekana kuwa kubwa kupita kiasi,” alisema.
Wakili wa utetezi, Patrick Kabou, pia alieleza hukumu hiyo kuwa “isiyoeleweka”, akidai mashabiki hao ni waathirika.
Mahakama ya Morocco imewahukumu mashabiki 19 wa soka kifungo cha mwaka mmoja jela kwa vitendo vya kihuni walivyovionesha wakati wa mchezo wa fainali ya AFCON 2025 kati ya Morocco na Senegal, ambapo walijaribu kuvamia uwanja.
Baada ya kikao cha mahakama kilichodumu kwa zaidi ya masaa matano, Jaji aliyekuwa akiongoza kesi hiyo aliamua kuwa mashabiki hao, raia 18 wa Senegal na mmoja wa Ufaransa, walikuwa na hatia ya zaidi ya mashtaka sita, yakiwemo ya kuharibu miundombinu ya uwanja wa michezo na kufanya vurugu wakati wa tukio la michezo.
Kwa mujibu wa Wakili Naima El Guellaf, mashabiki 11 wamehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na kutozwa faini ya dola 550. Wanne wengine wamehukumiwa kifungo cha miezi sita na faini ya dola 218. Na wanne waliobaki wamehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela na faini ya dola 130.