MOROGORO: MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha utoaji vibali vya kuajiri askari wa wanyamapori takribani 551 kwa mwaka wa fedha  2025/26.

Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Yussuf Kabange amesema hayo kwenye ziara ya  wajumbe wa Bodi ya Nne ya Mamlaka hiyo ilipotembelea Makao makuu wa Tawa kwa muda wa siku mbili  mjini Morogoro.

Bodi ya wakurugenzi hiyo inaongozwa na Mwenyekiti wake Meja Jenerali Mstaafu , Hamis Semfuko, ambapo pia aliwavisha  vyeo vya kijeshi Makamishna wa Uhifadhi  13 katika hafla ya Kijeshi iliyofanyika  katika Ofisi za TAWA Makao Makuu, Mkoani Morogoro.

Hivyo askari hao wataenda kuongeza nguvu katika uzimamizi wa ulinzi wa rasilimali wanyamapori.

“Maono ya bodi  ya nne kwa kifupi tumeambiwa  inataka kuiona TAWA  inapaa na kuwa na ubora wa viwango vya utendaji kazi katika kazi za uhifadhi,  kazi za utalii , kuvutia wawekezaji kushirikisha wananchi katika viwango vyote “amesema Kabange.

Kabange amesema utokana na malekezo ya Serikali, Waziri pamoja na  bodi hiyo na maono yake ya kuiona Tawa inapaa, Menejimenti ya Mamlaka hiyo imejipanga katika utendaji kazi wake kwa ufanisi mkubwa.

Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Kurugenzi ya Huduma za Shirika, Maarufu Thabit Mkwaya, amesema katika siku za hivi karibuni Mamlaka hiyo imepata  askari wapya 296 .

Mkwaya amesema askari hao wanaenda kuongeza tija kwenye utendaji kazi wa Mamlaka na kwamba viongozi waliovalishwa na kupandishwa vyeo  wao wanakwenda kwenye ngazi za kanda kwa maana ya viongozi wa kanda za Tawa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi  ya Wakurugenzi ,  Semfuko amewapongeza  Makamishna kwa kuaminiwa na Bodi ya Wakurugenzi na kuteuliwa nafasi hizo katika maeneo mbalimbali ya usimamizi.

“Ninawapongeza Makamishna wote 13 waliotunikiwa na kuvishwa vyeo, ni imani ya Bodi kuwa mnastahili vyeo hivyo, hongereni ,” amesema  Mwenyekiti wa Bodi Semfuko.

Amewataka kwenda kutekeleza maelekezo ya Serikali na maono ya bodi ya nne kwa  kuhakikisha Mamlaka hiyo  inapaa katika viwango vyote vya utendaji kazi ikiwemo ushirikishaji wa jamii, usimamizi wa kazi za uhifadhi, kuendeleza utalii, kuongeza uwekezaji na ukusanyaji wa mapato.

“Tunataka tuone TAWA inapaa juu zaidi na nyinyi ndio moja ya vichocheo vya kufanya hivyo,” amesema Semfuko.

Pia amewataka Makamishna wa uhifadhi kwenda kufanya kazi kwa kushirikiana na Maafisa na Askari walio chini yao kwa kuzingatia miongozo iliyopo huku wakizingatia ubunifu, weledi, sheria na utu.

Katika hafla hiyo Makamishna wa Uhifadhi waliovishwa vyeo ni Makamishna Wasaidizi Waandamizi  ni saba ambao ni Privatus Kasisi, Wilbright Munuo, Khadija Malongo, Mark Chuwa, Vicky Kamata, Omary Msangi na Orest Njau.

Kwa upande wa  Makamishna Wasaidizi  ni sita ambao ni Alphonce Mung’ong’o, Jackson  Msaki, Suleiman Keraryo, Jovine Nachihangu, George  Makheya na Rajabu Hochi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *