Iringa. Safari ya Tumaini Msowoya ni mfano wa mwanamke aliyegoma kukata tamaa na kuamua kugeuza changamoto kuwa fursa.

Hii ni kwa jinsi anavyochanga karata zake kuitafuta kesho iliyo bora, akianza na taaluma ya uandishi wa habari kisha siasa na biashara.

Tumaini aliwahi kufanya kazi katika Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kama mwandishi wa habari.

Baadaye aliamua kujikita zaidi katika siasa na sasa ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Iringa. Amewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani humo na Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa.

Lakini nje ya siasa, Tumaini ni mjasiriamali anayejitegemea. Anaendesha kampuni ya ufuaji nguo iitwayo Jaira Dry Cleaner pamoja na miradi ya kilimo cha maua, matunda na mbogamboga katika eneo la Kihesa, Manispaa ya Iringa.

Mama wa watoto wawili na mlezi wa watoto wa hiari, pia ni mwimbaji wa nyimbo za injili. Kupitia biashara yake, ameajiri vijana saba, akiwemo meneja mmoja.

Mwanzo wa safari mpya

Mwaka 2019 hadi 2020, wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Uviko – 19, Tumaini alikuwa miongoni mwa wafanyakazi waliopunguzwa kazini.

Badala ya kukata tamaa, anasema aliamua kurejea Iringa na kuanza upya. Alifuatilia mafao yake kwa miezi kadhaa, alipoyapata aliyaweka benki huku akitafakari hatua inayofuata.

Wazo la kuanzisha biashara ya ufuaji nguo lilizaliwa wakati akiwa Njombe. Alipoenda kufua nguo katika moja ya ‘dry cleaner’, alipata hamasa ya kujiuliza kama naye angeweza kufanya biashara hiyo.

Baada ya mazungumzo na mmiliki wa biashara hiyo, aliamua kufanya utafiti wa kina.

Alitembelea dry cleaner mbalimbali zilizoko eneo la Njombe mjini, Dar es Salaam na Iringa na huko ndiko alikojifunza namna zinavyoendeshwa.

Alipojiridhisha, anasema alichukua vijana wawili na kuwapeleka Njombe kupata mafunzo maalumu. Kisha akatumia mafao yake kununua mashine na vifaa vingine muhimu, akaanzisha ofisi yake ya ufuaji nguo na akaipatia jina la Jaira Dry Cleaner.

Tumaini anasema mwanzoni haikuwa rahisi. Hata hivyo, taratibu wananchi walianza kuifahamu na kuzoea huduma hiyo. Leo hii, biashara imekua na imetoa ajira kwa vijana saba.

Tofauti na wengine, Tumaini anasema yeye alilenga kuwahudumia watu wa kipato cha chini kama madereva bodaboda na mama lishe. Wakati sehemu nyingine, koti linaweza kufuliwa kwa Sh5,000, Jaira Dry Cleaner hutoza takribani Sh2,000.

Lengo lake lilikuwa kutatua tatizo la uchafu kwa gharama nafuu, akiamini kuwa mtaji si fedha tu, bali ni wazo la kutatua changamoto iliyopo.

Mbali na ufuaji, anaendesha kilimo cha mazao ya asili kama magimbi na viazi vitamu, akiamini kuwa watu wengi wanapenda vyakula vya asili.

Bustani yake ya maua, matunda na mbogamboga imekuwa sehemu ya uzalishaji na pia mfano wa ubunifu wa kutumia rasilimali zilizopo.

Ndoto ya uandishi bado inaishi

Ingawa aliondoka katika ajira ya uandishi, Tumaini anasema hajaiacha taaluma hiyo moja kwa moja. Ameanza maandalizi ya kuendesha chombo cha habari cha mtandaoni. Anasema pamoja na kuwa na taaluma hiyo, pia amegeukia utunzi wa vitabu.

Mpaka sasa, anasema ameshaandika vitabu viwili, ‘Ujue uvulana wako’, kinacholenga kuwasaidia wazazi na walezi kuwalea na kuwaelekeza watoto wa kiume na ‘Ishi ndoto yako’, kinachohamasisha jamii kujiamini na kufuata ndoto zao.

Kupitia maandishi na mafunzo, mjasiriamali huyo anaamini kuwa kumuinua mtoto mmoja kwa elimu na maadili ni sawa na kupanda mbegu ya taifa bora.

 “Na katika hili, matokeo yake mtu hawezi kuyaona mara moja, lakini huja kwa hatua na uhakika zaidi,” anasema.

Siasa na kujiamini

Katika uwanja wa siasa, Tumaini amekua hatua kwa hatua. Anakiri kuwa awali hakuwa na ujasiri wa kuhutubia mbele za watu, lakini leo anaweza kuzungumza kwa zaidi ya dakika 60 bila hofu.

Anasema woga ni miongoni mwa vikwazo vinavyowarudisha nyuma watu wengi na kwamba, amejifunza kukimbilia fursa badala ya kuzikimbia.

Anasisitiza kuwa nafasi za uongozi si za kundi fulani maalumu, bali ni kwa yeyote mwenye uwezo, nidhamu na nia ya kuwatumikia wananchi.

Tumaini anasema ameendelea kufanya siasa bila kuchanganya maadili yake na mambo mengine, akiamini kuwa heshima ya mwanamke ni muhimu kuliko mafanikio ya haraka.

Ujumbe kwa wanawake

Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, Tumaini anatoa wito kwa wanawake kupambana na utegemezi na kukataa kubweteka.

“Binafsi ninaamini kwamba changamoto za maisha au hata kupoteza ajira si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa ukurasa mpya, ndivyo nilivyofanya mimi, nimefunua ukurasa mpya wa kitabu cha maisha yangu na sasa ninasonga mbele nikiwa si peke yangu, bali nikiwa na wasaidizi niliowaajiri,” anasema Tumaini kwa ujasiri.

Anapinga vikali rushwa ya ngono katika ajira na uongozi akisema mara zote anaamini kuwa kazi ni haki inayopatikana kwa uwezo na juhudi, si kwa kuuza utu.

Kwa uzoefu wake, anasema amefikia mafanikio bila kutumia njia zisizo sahihi na ameheshimiwa kwa misingi ya uwezo wake.

Pia, anawahimiza wanawake kuacha kutumia muda mwingi kwenye mazungumzo yasiyo na tija au udaku mitandaoni, badala yake wajifunze, wasome na kutafuta maarifa yatakayowaongezea thamani.

Zaidi ya mafanikio yake binafsi, Tumaini amejikita katika kuwainua wengine. Anasema ajira saba alizozitoa si takwimu tu, bali ni maisha ya vijana waliopata heshima na matumaini mapya. Kupitia mafunzo ya uandishi na ujasiriamali, anasema anajenga kizazi kitakachoweza kujitegemea.

Hadithi yake inaonyesha kuwa mafanikio si mstari ulionyooka. Ni mfululizo wa uamuzi mgumu, majaribio na kuanguka kisha kusimama tena.

Kutoka kupoteza ajira hadi kuanzisha biashara, kutoka kuogopa kuhutubia hadi kuwa kiongozi wa kisiasa, Tumaini amevuka viunzi vingi vya maisha.

Kwa ujumla, safari ya Tumaini Msowoya ni ushahidi kuwa mwanamke anapojitambua na kuamua, anaweza kubadilisha maisha yake na ya wengine. Kupitia uandishi, siasa na biashara, ameonyesha kuwa ndoto hazifi isipokuwa pale mtu anapoacha kuziamini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *