Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa, huenda likasitisha msaada na harakati zake za kibinadamu nchini Somalia ifikapo mwezi Aprili mwaka huu sababu ni ufadhili mpya kutopatikana haraka.

WFP imesema hatua hiyo itawaweka mamilioni ya watu nchini Somalia katika hatari kubwa ya kukabiliwa na baa la njaa. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa lenye makao yake makuu mjini Roma Italia limesema kuwa, tayari limelazimika kupunguza idadi ya watu wanaopokea msaada wa dharura wa chakula kutoka milioni 2.2 mwanzoni mwa mwaka huu wa 2026 hadi kufikia watu 600,000.

Shirika hilo limesema kuwa, inakadiriwa kuwa watu milioni 4.4 wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula, huku wengine karibu milioni moja kati yao wakikumbwa na viwango vya juu vya njaa, hasa kutokana na athari za uhaba wa mvua, migogoro na kupungua kwa ufadhili.

Ross Smith, mkurugenzi wa mipango wa WFP anayeshughulikia pia hali za dharura amesema hali inazidi kuwa mbaya na kwa kiwango cha kutisha huko Somalia na kwamba familia nyingi zimepoteza kila kitu na sasa zinaelekea kwenye janga kubwa ikiwa hakutapatikana msaada wa haraka wa chakula.

Mwezi Novemba mwaka 2025, Somalia ilitangaza hali ya dharura ya kitaifa kufuatia ukame ulioshuhudiwa baada ya misimu ya mvua isiyotabirika huku nchi zingine katika eneo hilo zikiripotiwa pia kuathiriwa kama alivyoeleza Mkuu wa WFP huko Turkana nchini Kenya akisema kuwa idadi ya watu wanaohitaji usaidizi ni 333,000 lakini ufadhili uliopo hautoshi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *