
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kuimarisha juhudi za uwezeshaji wa vijana kiuchumi nchini, Vijana wa chama ACT-Wazalendo wameibua kasoro kadhaa wakipendeza mambo manne kumaliza changamoto za vijana nchini.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Jumatatu Februari 23, 2026, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo, Abdul Nondo, ameshauri mabadiliko ya kimuundo katika usimamizi wa Sh200 bilioni zilizotolewa kwa ajili ya vijana, akisema bila mifumo imara fedha hizo hazitawanufaisha vyama walengwa.
Novemba 14,2025 akilizindua Bunge jijini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan alisema awamu yake ya pili ya uongozi Serikali imejipanga kuwezesha vijana kikamilifu.
Katika kuweka mifumo ya uwezeshaji bora wa vijana, Rais Samia aliunda Wizara maalumu ya Maendeleo ya Vijana ndani ya ofisi yake na kuipa maelekezo ya namna ya kulisaidia kundi hilo.
“Tumeamua kuwa na wizara kamili itakayoshughulikia mambo ya vijana na kuwa na washauri wa vijana ndani ya ofisi ya Rais badala ya kuwa na idara ndani ya wizara yenye mambo mengi na kuangalia njia nzuri ya kunufaisha vijana,” alisema Rais Samia.
Aidha aliweka wazi Serikali imetenga Sh200 bilioni kwa vijana na wanawake ili kuongeza mitaji na kutoa mikopo nafuu kwa makundi hayo akitilia mkazo Serikali itaendelea kufungua madirisha ya mikopo nafuu kwa kushirikiana na sekta binafsi nchini.
Katika hoja zake mbele ya waandishi wa habari leo Jumatatu, Nondo amesema licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali bado hakuna uwazi wa kutosha kuhusu wapi la kuzipata, utaratibu wa utoaji, usimamizi na urejeshwaji wake kwa vijana.
“Tunapendekeza kiundwe chombo maalumu bungeni kiitwe Wakala wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (Tanzania Youth Empowerment Agency -TYEA) kitakachosimamia uratibu, utoaji na udhibiti wa fedha za vijana kuanzia ngazi ya taifa hadi wilaya,” amesema.
Amefafanua wakala huo uwe na Mkurugenzi wa Taifa, bodi na idara zake, kisha ushuke hadi mikoa na wilaya ili vijana wapate huduma sehemu moja badala ya fedha kusambazwa kwenye wizara za kisekta bila maelezo ya wazi.
Pendekezo la pili, amesema, ni kutungwa kwa sheria rasmi ya mfuko wa maendeleo ya Vijana badala ya kuendelea kutumia mwongozo wa mwaka 2022 wenye kurasa 12 pekee.
Pendekezo la tatu ni kusitisha utaratibu wa asilimia nne ya mapato ya halmashauri kusimamiwa kienyeji, badala yake fedha hizo zipelekwe moja kwa moja kwenye mfuko wa vijana chini ya wakala huo maalumu.
Nne, ametaka Wizara ya Maendeleo ya Vijana ibebe kikamilifu jukumu la kuratibu na kusimamia sera na mifumo, huku wizara za kisekta zikibaki na kazi ya kuibua fursa pekee badala ya fedha za vijana kupelekwa katika wizara hizo, hali inayodunisha uwezo wa Wizara ya Vijana kudhibiti na kuratibu uwezeshaji huo.
Februari 5, 2026 akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya hundi ya fedha hizo kwa Waziri wa Vijana, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba aliweka wazi nia ya Serikali kuhakikisha fedha hizo zinawanufaisha vijana akiagiza kuwekwa masharti nafuu.
Akitoa takwimu, Nondo amesema kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya 2022, vijana ni asilimia 70 ya Watanzania na wanachangia asilimia 56.6 ya nguvu kazi, huku vijana 200,000 tu kati ya 1,000,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka hupata ajira, 800,000 wakibaki bila fursa rasmi.
Akirejea Takwimu za Nguvu Kazi (Intergreted Labour Force Survey 2021), Nondo amesema asilimia 80 ya vijana wapo sekta isiyo rasmi, wengi wakikosa mikopo ya benki kwa kukosa dhamana.
“Mimi nafanya biashara ya viazi, nilitaka mkopo wa Sh10 milioni benki, nilitakiwa kurejesha Sh24 milioni kwa mwaka mmoja huku benki wanataka dhamana ya nyumba au gari ambazo sina, nilishindwa,” amesema.
Amekosoa pia uamuzi wa fedha hizo kupitishwa kwenye wizara mbalimbali badala ya kuingia moja kwa moja kwenye mfuko wa vijana, akisema hali hiyo imeongeza uwezekano wa urasimu, hofu ya upendeleo na hata kurejeshwa serikalini baadaye kwa kisingizio cha kukosa wakopaji.
“Sh200 bilioni ni fedha nyingi sana. Tunataka mifumo ya wazi, taarifa za wazi na usimamizi madhubuti ili vijana wanufaike wapewe taarifa za kutosha na kunufaika kwa usawa,” amesisitiza.
Hata hivyo, Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, ameshaweka wazi na amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa wizara hiyo imejizatiti kuhakikisha fedha hizo zinatolewa kwa usawa, na Serikali imetoa kipaumbele cha kipekee kwa vijana katika mikakati yake.
Alipozungumzia siku 100 za Rais Samia Ikulu, Februari 14, 2026 Waziri Nanauka, alisema Serikali imejizatiti katika kuwawezesha vijana akiweka wazi kuwa wizara yake inahakikisha kila kijana anapata nafasi sawa katika fursa zote zilizopo ndani ya wizara hiyo.