Dodoma. Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) kimezindua Mradi wa Kikohozi Classifier, unaotumia teknolojia ya akili unde (AI) kubaini mapema kifua kikuu na magonjwa ya mfumo wa hewa ili kuwaunganisha na huduma stahiki za afya.

Mradi huo wa kujitolea utatekelezwa katika mikoa ya Iringa, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Shinyanga na Dodoma, huku Dodoma ikihusisha wilaya za Bahi na Dodoma Jiji. Waendeshaji wa mradi huo wamesema utekelezaji wake unachangia Lengo la Tatu la Maendeleo Endelevu (SDGs) linalohusu afya bora na ustawi wa watu wote.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo leo Jumatatu, Februari 23, 2026, Mkuu wa Shule ya Uuguzi na Ukunga Afrika Mashariki wa AKU, Profesa Eunice Ndirangu amesema mradi huo umeidhinishwa na Wizara ya Afya pamoja na Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma.

Amesema ubunifu huo unaimarisha ushirikiano wa kitaifa katika kuendeleza tafiti na suluhisho bunifu za afya, akisisitiza mafanikio ya mradi yanategemea mshikamano wa wadau mbalimbali.

“Ushirikiano ni muhimu kwa utekelezaji endelevu wa utafiti. Washirika wetu wanaleta utaalamu, uzoefu na nguvu katika maombi ya ruzuku, afua za utafiti na ushirikishwaji wa Serikali, jambo linalochochea lengo la nchi la kuhimiza ubunifu katika sekta ya afya,” amesema Profesa Ndirangu.

Mratibu na msimamizi wa mradi huo, Dk Kahabi Isangula amesema Kikohozi Classifier inalenga kuimarisha mifumo ya ugunduzi wa mapema wa magonjwa ya mfumo wa hewa ili kupunguza vifo, kuboresha ubora wa maisha na kupanua upatikanaji wa huduma za afya nafuu zinazolingana na mahitaji ya jamii husika.

Amesema hatua ya sasa ni ya majaribio huku akiwahimiza wasaidizi wa utafiti kuzingatia weledi, usahihi na uadilifu katika ukusanyaji wa takwimu ili matokeo yatakayopatikana yasaidie upanuzi wa mradi huo katika maeneo mengine nchini.

“Mafanikio ya awamu hiyo yatatoa msingi wa kupeleka afua hii kitaifa. Ni muhimu kuhakikisha takwimu tunazokusanya ni sahihi na zinaaminika,” amesema Dk Isangula.

Makamu Mkuu wa AKU Tanzania, Profesa Eunice Pallangyo amesema Tanzania inapaswa kujijengea uwezo wa kufanya tafiti zake kwa viwango vya kimataifa badala ya kutegemea tafiti kutoka nje.

“Tunapaswa kufanya tafiti zetu kwa weledi na kutoa matokeo yasiyo na shaka. Tukifanya hivyo, Tanzania inaweza kuwa mfano kwa mataifa mengine,” amesema Profesa Pallangyo.

Hata hivyo, Meneja wa Mpango wa Udhibiti wa Kifua Kikuu na Ukoma wa Wizara ya Afya,  Dk Kisonga Riziki amesema kifua kikuu bado ni janga.

Amesema tatizo litakuwa kubwa kwa siku za usoni kutokana na kugundulika kwa madini na kuongeza idadi ya wachimbaji.

Dk Riziki amewaomba AKU kufanya kazi kwa umakini kama walivyoamua kwa kuwa,  wanaweza kulisaidia Taifa.

Amesema mradi huo ni mkombozi kwa magonjwa hayo huku akiomba timu ya ukusanyaji taarifa iwe makini ili kutoa matokeo chanya.

Dk Riziki amesema maeneo ya uchimbaji madini yanaweza kuwa sehemu ya kichocheo cha magonjwa hayo, hivyo inatakiwa kuangaliwa na elimu zaidi ipelekwe huko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *