Harakati ya Ansarullah ya Yemen imelaani vikali “mauaji ya umati ya umwagaji damu” yaliyofanywa na utawala wa Israel katika eneo la Beqaa mashariki mwa Lebanon, na kuuwa takriban watu kumi na kujeruhi wengine wengi.

 Ansarullah imeyataja mauaji hayo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa thamani za kibinadamu na mikataba ya kimataifa.

Idara ya Kisiasa ya harakati ya Ansarullah jana Jumapili ilisema katika taarifa yake kuwa mashambulizi ya anga ya Israel yaliyokilenga kitongoji ndani ya kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Ain al Hilweh katika mji wa Sidon kusini mwa Lebanon yamefanywa katika fremu ya ajenda za kujitanua za Israel.

Taarifa ya Ansarullah imeongeza kuwa: Jinai hiyo ni zaidi ya kushambulia raia wa Lebanon na kukiuka mamlaka ya kujitawala nchi hiyo. Ansarullah imetaja jinai za Israel dhidi ya Lebanon kuwa ni sehemu ya majaribio ya hatua mpya zinazohusishwa na kile kinachotajwa kama mkakati wa  “Israeli Kubwa” na “Mashariki ya Kati Mpya.”

Harakati ya Ansarullah ya Yemen imesema inawaunga mkono kikamilifu wananchi wa Lebanon na harakati ya Hizbullah dhidi ya chokochoko za Israel zinazoungwa mkono na  Marekani na nchi nyingine za Magharibi. 

Wizara ya Afya ya Umma ya Lebanon Jumamosi ilitangaza kuwa watu 10 wameuawa na 24 kujeruhiwa, wakiwemo watoto watatu, katika mashambulizi ya anga ya Israel mashariki mwa Lebanon. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *