Tanga. Bei ya magimbi na viazi vitamu zimeendelea kupanda katika soko la Mgandini jijini Tanga, hali inayowaathiri wananchi wanaotegemea vyakula hivyo kwa ajili ya futari katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma.
Leo Jumatatu Februari 23, 2026, Mwananchi limetembelea soko hilo na kuzungumza na wafanyabiashara wa viazi vitamu, magimbi, nazi na viazi mbatata ambavyo hutumika kwa wingi kuandaa futari na kubaini ongezeko la bei kwa vyakula hivyo.
Mfanyabiashara wa viazi vitamu na magimbi, Rehema Abdalah amesema zamani alinunua gunia la viazi vitamu kwa kati ya Sh30,000 hadi Sh50,000, lakini kwa sasa analinunua kwa Sh180,000.
“Gunia la viazi vikubwa nalinunua Sh180,000 na la viazi chenga Sh70,000, bado nauli ni Sh20,000. Zamani nilikuwa nachukua magunia 30, lakini sasa napata magunia matano hadi 10 kulingana na mtaji wangu,” amesema Rehema.
Bidhaa ya viazi vitamu inayotajwa kupanda bei katika msimu huu wa Ramadan na Kwaresma.
Mfanyabiashara mwingine, Zawadi Muya amesema hali ya biashara mwaka huu ni tofauti na mwaka jana.
“Mteja akiona fungu la magimbi la Sh3,000 au Sh5,000 anaondoka wakati mwaka jana alikuwa ananunua bila malalamiko. Safari hii kumekuwa kugumu sana,” amesema Muya.
Mkazi wa Mabawa, Tanga, Amina Ally, amesema kupanda kwa bei kumewaongezea ugumu wa maisha wananchi wengi.
“Bei zimepanda tofauti na mwaka jana, tunalazimika kununua kwa kiasi kidogo ili kukidhi mahitaji ya familia,” amesema Ally.
Kwa upande wa nazi, wafanyabiashara wamesema bei zake haijapanda, lakini upatikanaji wake umekuwa mgumu kutokana na uhaba wa uzalishaji wa ndani.
Mfanyabiashara wa nazi, Omari Salimu amesema nazi nyingi kwa sasa zinatoka Mombasa, Kenya kutokana na ukame uliosababisha uzalishaji
Mfanyabiashara mwingine wa nazi, Rehema Sadiki amesema changamoto kubwa ni jamii kutegemea minazi ya urithi bila kupanda mipya.
“Tukibadilika na kuanza kupanda minazi mipya na kutunza mashamba yetu, hatutakuwa na uhaba wa nazi kila inapofika Ramadhani,” amesema Sadiki.
Wafanyabiashara wa nazi katika solo la Mgandini wakiendelea kuhudumia wateja wanaotumia soko hilo kujitafutia mahitaji ya chakula.
Mkazi wa Tanga, Alfonce Njelekela amesema ni muhimu kuongeza upandaji wa minazi ili kukabiliana na changamoto hiyo.
“Tuna ardhi inayofaa kwa minazi, lakini hatuongezi upandaji. Hiyo ndiyo sababu ya uhaba wa nazi unaojitokeza mara kwa mara,” amesema Njelekela.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa viazi mbatata, Pascal Kashamba amesema bei ya viazi hivyo ilipanda mwishoni mwa mwaka 2025, lakini sasa imeanza kushuka kidogo kutokana na upatikanaji kutoka mikoa mingine.
“Kwa sasa bei imeanza kushuka tofauti na ilivyokuwa Desemba 2025, hivyo angalau kuna nafuu kidogo sokoni,” amesema Kashamba.
Akizungumzia suala la kupanda kwa bei, Makamu Mwenyekiti wa Soko la Mgandini, Akida Zumo amesema mabadiliko ya bei yanatokana na mahitaji na upatikanaji wa bidhaa.
“Kipindi hiki mahitaji ni makubwa, lakini kwa ujumla mfumuko wa bei si mkubwa sana isipokuwa kwa baadhi ya bidhaa,” amesema Zumo.
Kwa ujumla, hali ya soko la Mgandini jijini Tanga inaonyesha mchanganyiko wa changamoto za upatikanaji na kupanda kwa bei za baadhi ya mazao muhimu, hususan magimbi na viazi vitamu, jambo linaloongeza mzigo kwa wananchi katika kipindi hiki cha mfungo wa Kwaresma na Ramadhani.