DAR ES SALAAM: Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO), Lazaro Twange, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya umeme inayotekelezwa mkoani Simiyu.
Lengo lilikuwakujionea maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kusambaza Umeme cha Imalilo pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 (220kV) kutoka Shinyanga hadi Simiyu.
Akizungumza mara baada ya ziara, Twange alisema mradi wa kituo cha Imalilo ulianza kutekelezwa mwezi Oktoba 2025 na wataalamu wa ndani wa Shirika, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 2026.

“Baada ya muda mrefu tumeanza kutekeleza mradi huu kupitia wataalamu wetu wa ndani ambapo tulianza mwezi Oktoba 2025, na tunatarajia kuukamilisha mwezi Mei 2026,” alisema Twange.
Alifafanua kuwa kwa sasa wananchi wa Bariadi wanategemea umeme kutoka mikoa jirani ya Shinyanga, Mwanza na Mara, hali inayosababisha kupungua kwa ubora wa umeme kutokana na umbali mrefu unaosafiri.
Alisema kukamilika kwa Kituo cha Imalilo kutaondoa changamoto hiyo na kuimarisha miundombinu ya umeme, hivyo kuhakikisha wananchi wa Bariadi wanapata umeme wa uhakika kuanzia Juni 2026.
“Kwa sasa wananchi wa Bariadi wanategemea umeme kutoka mikoa ya Mwanza, Mara na Shinyanga, hali inayosababisha ubora wa umeme kupungua. Ujenzi wa kituo hiki utaimarisha miundombinu na kuondoa changamoto hizo kuanzia Juni 2026,” aliongeza.
Kwa sasa utekelezaji wa mradi wa Kituo cha Kupokea na Kusambaza Umeme cha Imalilo umefikia asilimia 20.75. Mradi huo unagharimu takribani Sh bilioni 8, fedha zinazofadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu ya kwanza