Kocha wa Manchester United, Michael Carrick, ametoa wito kwa kikosi chake kupambana kuhakikisha wanarejea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukaa nje ya mashindano hayo kwa miaka miwili.
United wamejiweka katika nafasi nzuri ya kumaliza ndani ya tano bora kufuatia kushinda mechi nne na kutoka sare moja katika michezo mitano ya Carrick tangu ateuliwe kuwa kocha wa muda hadi mwisho wa msimu.
Kufuzu katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kunaweza kuingizia klabu zaidi ya pauni milioni 100 (Sh347 bilioni).
Kiungo wa zamani wa Man United ambaye ni kocha wa muda wa timu hiyo akiwa amebeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya walilotwaa mwaka 2008 katika mechi ya fainali dhidi ya Chelsea. Picha na Mtandao
Carrick, ambaye aliwahi kutwaa Kombe hilo mwaka 2008 chini ya Alex Ferguson, amesema:
“Hapo ndipo tunapotaka kuwa. Tumewahi kupata mafanikio makubwa kwenye mashindano haya, na kwa sababu nyingi tofauti, ni sehemu tunayotamani kurejea. Inawezekana, na ni juu yetu kutumia nafasi hiyo.”
Ameongeza kuwa kikosi chake kina mtazamo chanya lakini hakipaswi kubweteka kwa matokeo ya hivi karibuni.
Kocha wa muda wa Man United, Michael Carrick (kulia), nahodha wa timu hiyo, Harry Maguire (kushoto) wakitoa shukrani kwa baadhi ya mashabiki wao katika Uwanja wa Old Trafford. Picha na Mtandao
“Tuko katika nafasi nzuri, ingawa ningependa tuwe katika nafasi bora zaidi. Inawezekana, lakini ni juu yetu kutumia fursa hiyo,” amesisitiza.
Kuhusu mmiliki mwenza wa klabu, Jim Ratcliffe, Carrick amesema mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Arsenal mwezi uliopita, na hakuhisi kuna haja ya mawasiliano ya mara kwa mara kutoka juu ya uongozi.
“Jukumu langu ni kuunda mazingira mazuri ndani ya kikosi na kuongoza timu. Sihitaji mawasiliano ya kila mara kutoka juu,” amesema Carrick.
Uwanja wa Everton, Hill Dickinson unaobeba idadi ya watazamaji 52,769 ambapo leo saa 5:00 usiku utapigwa mchezo wa Ligi Kuu England kati ya Everton na Man United. Picha na Mtandao
Leo Man United itakuwa na kibarua kingine ugenini mbele ya Everton ambayo itakuwa kwenye dimba lake la nyumbani la Hill Dickinson. Iwapo watafanikiwa kuondoka na ushindi katika mtanange huo, vijana wa Carrick watapanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi wakiishusha Chelsea ambayo wanalingana kwa pointi hadi sasa.