Dar es Salaam. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde  amepongeza ushirikiano wa kimkakati kati ya Benki ya CRDB na Tume ya Madini, akieleza kuwa, mpango maalumu wa kifedha uliozinduliwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ni hatua ya kihistoria itakayobadili mfumo wa upatikanaji wa mitaji katika sekta ya madini nchini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa huduma hizo na utiaji saini wa Mkataba wa Makubaliano (MOU) uliofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, Waziri Mavunde amesema sekta ya madini imeendelea kukua kwa kasi, ikichangia asilimia 10 ya Pato la Taifa na asilimia 56 ya mapato ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya nje yanayozidi Sh12.8 bilioni.

“Sekta ya madini sasa ni injini ya uchumi wetu. Tunachokishuhudia leo ni daraja linalounganisha maono ya Serikali na nguvu ya mtaji kutoka sekta ya fedha. Ushirikiano huu unaenda moja kwa moja kumgusa mchimbaji mdogo na kumwinua katika uchumi rasmi. Benki ya CRDB mmeonesha kuwa, ni benki kiongozi katika kuleta suluhisho stahiki kwa sekta mbalimbali. Tunawashukuru sana,” amesema Waziri Mavunde.

Amesisitiza kuwa, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imekuwa ikitekeleza mageuzi ya kisera, kiusimamizi na kisheria ili kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha Watanzania wengi zaidi, hususan wachimbaji wadogo.

Mpango uliozinduliwa na CRDB unaleta mageuzi makubwa katika mfumo wa dhamana kwa kutambua dhamana mbadala zinazotokana na shughuli za uchimbaji moja kwa moja.

Kwa mara ya kwanza katika sekta ya benki nchini, leseni halali za uchimbaji, mikataba ya mauzo ya dhahabu na akiba ya dhahabu iliyohifadhiwa katika viwanda vya kusafisha kwa pamoja inatambuliwa kama dhamana zinazokubalika kwa ajili ya mikopo.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema mpango huo ni mfumo kamili wa kifedha unaogusa mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini kuanzia uchimbaji, uchakataji, uhifadhi, usafirishaji hadi biashara na masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Huu ni muundo mpya wa kifedha unaotambua uhalisia wa sekta ya madini. Tumekubali dhamana zinazotokana na shughuli halisi za wachimbaji badala ya mali zisizohusiana na sekta. Hii itafungua milango kwa maelfu ya wachimbaji wadogo waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa kifedha,” amesema Nsekela.

Amesema mpango huo unajumuisha mikopo ya mtaji kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za uchimbaji, mikopo ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya kisasa, mikopo inayodhaminiwa na dhahabu, huduma za bima za migodi na wafanyakazi kupitia CRDB Insurance, pamoja na akaunti maalumu za miamala ya madini na dhahabu zitakazorahisisha ufuatiliaji na uwazi wa biashara.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi CRDB, Donald Mmari amemweleza Waziri wa Madini kuwa bodi imeweka miongozo ya kimkakati inayolenga kuhakikisha sekta ya madini inakua kwa kuzingatia misingi ya uendelevu, uwajibikaji na uchumi shirikishi.

“Tunataka kuona wachimbaji wadogo wanapanda ngazi kutoka uchimbaji wa jadi hadi kutumia teknolojia bora, kupata masoko rasmi na kushiriki katika uongezaji thamani. Ukuaji wa sekta ya madini lazima uwe endelevu na wenye manufaa kwa jamii,” amesema Dk Mmari.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji, Rais wa Chama cha Wachimbaji Madini Tanzania (Femata), John Bina amesema mpango huo umeleta matumaini mapya kwa wachimbaji wadogo waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukosa dhamana zinazokubalika na taasisi za fedha.

“Leo tunashuhudia mwanzo wa zama mpya. Wachimbaji wadogo tumepewa heshima ya kutambuliwa kama washirika halali wa maendeleo. Tunaishukuru sana Benki ya CRDB kwa kutuletea suluhisho hili,  tunawaahidi tutaendelea kushirikiana nao pamoja na Serikali kuhakikisha tunatumia fursa hii kwa uwajibikaji,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *