
Mkuu wa harakati ya Kiislamu ya Ennahda, Rached Ghannouchi, amesema kwamba mustakabali wa Tunisia ni uhuru, utawala wa sheria na kubadilishana madaraka kwa amani “hata kama itachukua muda.”
Haya yamekuja katika barua iliyoandikwa na Rached Ghannouchi, spika wa bunge lililovunjwa la Tunisia, kutoka gerezani huko Mornaguia karibu na mji mkuu Tunis, kwa wanachama wa harakati hiyo.
Katika ujumbe wake, Ghannouchi amesema: “Mataifa hayajengwi kwa kulazimishwa, wala hayaimarishwa na dhulma, bali yanategemea mashauriano, uadilifu na kuheshimu matakwa ya watu.”
Pia amesisitiza kwamba “demokrasia ni utaratibu wa amani wa kuhamisha madaraka na dhamana ya haki, na si mgeni katika roho ya Uislamu, bali inaendana na malengo yake makuu katika kuzuia udhalimu na kulinda hadhi na heshima ya mwanadamu.”
“Mustakabali wa Tunisia ni uhuru, hata kama itachukua muda. Mustakabali wake ni utawala wa sheria, taasisi, kuhamishwa madaraka kwa amani na kuheshimiwa utofauti,” amesema Rached Ghannouchi.
Ameeleza kwamba: “Njia zinaweza kuwa ngumu na barabara inaweza kuwa ndefu, lakini kanuni ya historia ni kwamba mataifa yaliyohai hayafi, na kwamba azma ya kupata uhuru haishindwi kamwe.”
Ghannouchi amewahutubu wanachama wa harakati ya Kiislamu ya Ennahda, akisema, “Simameni imara katika maadili na kanuni, na kuweni waaminifu kwa ukweli na uadilifu.”
Inafaa kuzingatiwa kwamba Ghannouchi amefungwa gerezani tangu alipokamatwa Aprili 17, 2023, baada ya nyumba yake kuvamiwa na askari usalama kwa madai ya “kufanya uchochezi dhidi ya usalama wa taifa.”