GEITA; HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Geita imeanzisha karakana ya macho ili kukabiliana na mahitaji ya huduma za macho ambayo yamezidi kuongezeka kwa watu wanaopitia changamoto hiyo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita, Dk Mfaume Kibwana ametoa taarifa hiyo katika hafla ya kupokea msaada wa vifaa vya matibabu ya macho kutoka taasisi ya KCCO.
Dk Mfaume amesema kupitia uwekezaji wa serikali na msaada wa KCCO, hospitali hiyo imepata vifaa vya uchunguzi, matibabu na upasuaji wa macho vyenye thamani sh milioni 130.
Amesema kwa kutumia ufadhili huo hospitali imeweza kufikia wanufaika zaidi ya 434 kuanzia mwezi Oktoba 2025 kati yao wagonjwa 54 walifanyiwa upasuaji wa macho.
Amesema kupitia karakana mpya ya macho kuna maboresho ambayo itasaidia kutengeneza miwani na kusaidia wahitaji wa miwani ya macho kuipata kwa wakati na gharama nafuu.
“Lakini pia watoto hawajawekwa mbali katika upatikanaji wa huduma hizi kuna mashine zimeletwa kusaidia kwa ajili ya uchunguzi wa watoto kuhusu magonjwa mbalimbali ya macho”, amesema.
Mratibu wa huduma za Macho mkoa wa Geita, Dk Anath Mussa amesema mkoa una vituo vinavyotoa kliniki za macho 9 na watalaamu 17 wanaotoa huduma za macho kwa mkoa mzima.
“Katika kitengo cha macho pekee kuanzia Julai hadi Desemba 2025 wamehudumia takribani watu 7,000 huku kliniki za macho zikihudumia watu takribani 5,000 na upasuaji 181 ukifanyika”, amesema.
Amesema hali ya uelewa juu ya changamoto za macho katika jamii zetu bado upo chini kwa sababu watu wengi hawaamini kwenye matibabu, wana Imani potofu na kukithiri kwa tatizo.

Ofisa Mratibu wa Miradi wa KCCO, Peter Kileo amesema taasisi hiyo imejizatiti kuendelea kuyafikia maeneo yote yenye changamoto ya huduma za macho ili kuisaidia jamii kupunguza tatizo.
Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Geita, Dk Yohana Kihaga amsema kati ya vituo 307 vya huduma za afya, vituo tisa vinatoa huduma za macho huku sit ani vya serikali na vitatu vya binafasi.
“Niwaombe watu wote ambao mtakuwa mnatumia hivi vifaa siyo kwamba hapa ni mwisho bali hapa ni mwanzo na kwenye kila hatua ya kuboresha huduma za macho tutaendelea kusaidia”, amesema Dk Kihaga.