
Kamanda wa jeshi la Iran amepuuzilia mbali mkusanyiko wa meli na ndege za kivita za Marekani katika eneo la Asia Magharibi zilizoshuhudiwa wiki chache za hivi karibuni na kuitaja kuwa hatua ya kimaonyesho” huku kukiwa na mvutano kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran na kwamba Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa jibu madhubuti kwa hila hizo za hali ya juu.
Brigedia Jenerali Mohammad Jafar Asadi ambaye ni Naibu Inspekta wa Makao Makuu ya Kati ya Jeshi ya Khatamul Anbiya amesema: Taifa letu linajua vyema kwamba meli na silaha nyingine ambazo sasa zimetumwa katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman zimekuwa zikisafiri katika sehemu mbalimbali za dunia kwa miaka mingi.
Ameongeza kuwa, kutumwa meli katika Ghuba ya Uajemi kumeingia katika awamu ya propaganda na kwamba jibu la kitendo hicho cha tamthilia lilitolewa vyema na Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ambaye alisema hivi karibuni kwamba “Bila shaka meli hiyo inayobeba ndege ni chombo hatari, lakini hatari zaidi kuliko chombo hicho ni silaha inayoweza kuzamisha meli hiyo chini ya bahari.”
Kamanda Mohammad Jafar Asadi amekumbusha namna maadui wa Jamhuri ya Kiislamu walivyoshindwa katika kipindi cha miaka 47 iliyopita dhidi ya nchi hii na kusema: Tunatumai kwamba wale wote wanaochochea vita kama Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na utawala wa Kizayuni wa Israel hatimaye watatokomea katika eneo la Asia Magharibi kama uvimbe wa saratani.
Brigedia Jenerali Mohammad Jafar Asadi ambaye ni Naibu Inspekta wa Makao Makuu ya Kati ya Khatamul Anbiya pia amesisitiza kuwa vikosi vya ulinzi vya Iran viko tayari kwa vita kwa ajili ya kuihami nchi na kwamba vitachukua hatua madhubuti na kwa nguvu zote kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
“Jibu la vikosi vya ulinzi mkabala wa makosa yoyote ya kimahesabu na hatua ya kipumbavu ya adui litakuwa kali sana ikilinganishwa na huko nyuma,” amesema Brigedia Jenerali Asadi.