Shinyanga. Dosari za kisheria wakati wa usikilizwaji wa kesi ndani ya kesi (trial within trial) katika kesi ya mauaji ya mtoto Steven Malimi (6), zimeifanya Mahakama ya Rufani nchini, kuamua kesi hiyo isikilizwe upya na Jaji mwingine.

Hii ni baada ya jopo la majaji watatu, Shaban Lila, Issa Maige na Latifa Mansoor, kukubaliana na sababu ya  sita ya rufaa iliyokatwa na Herman Babu, maarufu  Yesu, aliyekuwa amehukumiwa adhabu ya kifo kwa kumuua mtoto huyo.

Katika hukumu yao waliyoitoa Februari 20,2026 na hukumu hiyo kupatikana katika tovuti ya mahakama leo Februari 23,2026, majaji hao wamebatilisha adhabu hiyo ya kifo na mwenendo wa kesi ndani ya kesi baada ya utetezi kufunga ushahidi.

Hivyo wameamuru jalada la kesi hiyo kurudishwa Mahakama Kuu kanda ya Shinyanga, ili shauri hilo lisikilizwe kuanzia pale upande wa utetezi ulipofunga ushahidi wao katika kesi ndani ya kesi ili Jaji mpya atoe uamuzi kwanza.

Katika shauri hilo, upande wa mashitaka unadai kuwa mshtakiwa alimuua mtoto huyo Agosti 30,3016 katika nyumba ya kulala wageni (Guest House) iitwayo Safari iliyopo katika mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

Steven alikuwa ni mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya Msingi Nyamatare iliyopo Wilaya ya Msoma mkoani Mara.

Ushahidi ulikuwaje

Ushahidi wa mashahidi wanne wa Jamhuri, unadai kuwa mtoto Steven alikuwa akiishi na mama yake mzazi, Mariam Steven aliyekuwa shahidi wa kwanza wa Jamhuri pamoja na shangazi yake na alikuwa akisoma Shule ya Msingi Nyamatare.

Katika ushahidi wake, Mariam alidai kuwa Agosti 26,2016 saa 2:00 asubuhi akiwa kazini na akiamini mtoto yuko shule, alipigiwa simu na Babu au Yesu ambaye alikuwa rafiki yake wa kiume wa zamani, kuwa amemchukua mtoto shuleni.

Alimweleza kuwa amemchukua mtoto huyo na anampeleka hotelini kula chakula, taarifa hiyo ilimshtua hivyo akaamua kwenda shuleni kuulizia juu ya taarifa hiyo, lakini walimu wakamjulisha mwanaye hakuwa amefika shuleni siku hiyo.

Hivyo yeye pamoja na ndugu zake walianza kumtafuta mshtakiwa na pia kupiga namba ya simu aliyoitumia kumpigia lakini hawakufanikiwa kumpata,  ndipo Agosti 27,2016 aliamua kutoa taarifa ya suala hilo katika kituo cha Polisi Musoma.

Katika kipindi hicho pia, alidai mahakamani kuwa alipokea simu kutoka kwa Babu au Yesu akimtishia kuwa angemuua ambapo Septemba 1,2016 alipokea simu ya Babu akimtaka aende Bariadi kuchukua mwili wa mtoto wake.

Baada ya kupokea simu hiyo, alidai akiwa na dada yake aitwaye Zawadi Steven, walikwenda kituo cha Polisi Bariadi na kuwaelezea na ndipo polisi waliwajulisha jana yake kuna mtoto alikuwa ameuawa na maiti ipo Hospitali ya Somanda.

Walikwenda hospitali hiyo na kutambua mwili wa mtoto ambapo kwa upande wa shahidi wa pili, Aziz Adamu ambaye ni muhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Safari, alidai Agosti 29,2016, mshtakiwa alifika akiwa na mtoto na kuchukua chumba.

Kulingana na shahidi huyo, mshtakiwa ambaye alifika hapo jioni, alijiandikisha katika kitabu cha wageni kwa jina la Herman Babu, maarufu Yesu.

Shahidi huyo alidai kuwa siku iliyofuata, mgeni huyo aliondoka bila kuwa na mtoto aliyekuja naye na wakati anafagia aligundua chumba alicholala mgeni huyo kilikuwa wazi na alipoingia alikuta mwili wa mtoto akiwa kitandani.

Mwili huo ulikuwa umefunikwa na shuka lililokuwa na matone ya damu, hivyo akatoa taarifa polisi ambapo mkaguzi msaidizi wa Polisi, Vedastus aliyekuwa shahidi wa nne na Dk Jumanne Lugata, shahidi wa tatu walifika eneo hilo.

Katika ushahidi wake, Dk Lugata aliyeufanyia uchunguzi mwili wa mtoto huyo, alidai sababu za kifo chake ilitokana na kunyongwa, ingawa hata hivyo ripoti yake haikupokelewa kama kielelezo kutokana na sababu za kiufundi.

Utetezi wa mshtakiwa

Kulingana na ushahidi, mshtakiwa alikamatwa huko Bunda Wilaya ya Musoma Septemba 2, 2016 na kusafirishwa hadi Bariadi siku iliyofuata ambapo alihojiwa na shahidi wa nne na kudaiwa alikiri kumuua mtoto Steven huko Bariadi.

Licha ya kukataa maelezo hayo na kusikilizwa kwa kesi ndani ya kesi, maelezo ya ungamo husika yalikubaliwa kuwa ushahidi na kutambuliwa kama kielelezo P1 kwa maelezo kwamba sababu za uamuzi huo, zitajumuishwa katika hukumu.

Katika utetezi wake, mshtakiwa alikanusha kutenda kosa hilo na kushikilia msimamo kuwa maelezo hayo ya ungamo yalipatikana baada ya kuteswa na siku ya tukio, hakuwa eneo la tukio bali alikuwa yuko Bunda.

Baada ya kushawishika na ushahidi wa shahidi namba moja na mbili, Jaji Seif Kulita wa Mahakama Kuu kanda ya Shinyanga alimtia hatiani mshtakiwa na kwamba ndiye anahusika na mauaji ya mtoto huyo na kumuhukumu kunyongwa hadi kufa.

Hoja za kisheria

Hakuridhishwa na hukumu hiyo hivyo akakata rufaa akiwasilisha sababu sita ambapo alidai Jaji alikosea kumtia hatiani kwa kuegemea maelezo ambayo hakuyatoa kwa hiari na yalichukuliwa nje ya muda.

Katika rufaa yake, mrufani aliwakilishwa na mawakili wa kujitegemea watatu, Ndurumah Majembe, Kassim Gila na Augustine Ijani wakati Jamhuri iliwakilishwa na mawakili waandamizi wa Serikali, Sophia Mgassa na Nancy Mushumbusi.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Wakili Gilla alieleza kuwa licha ya mrufani kupinga maelezo yake kuwa hakuyatoa kwa hiari na kesi ndani ya kesi kuendeshwa, Jaji alitoa uamuzi mdogo wa kulikataa pingamizi hilo la mrufani.

Katika uamuzi wa kesi ndani ya kesi, Jaji Kulita alitoa uamuzi wa kulikataa pingamizi la mrufani na kupokea maelezo hayo kama kielelezo na kuahidi angetoa sababu za kufanya hivyo kwenye hukumu, lakini haikuwa hivyo.

Wakili Gilla akaeleza kuwa kutotolewa kwa uamuzi wa kesi ndani ya kesi kabla ya mrufani kuanza kujitetea, kulifanya hoja ya kuteswa isipate majibu kwanza.

Hata hivyo, wakili mwandamizi wa Serikali Mgasa alipinga hoja ya maelezo kuchukuliwa nje ya muda akisema alikamatwa Septemba 2,2016 Bunda na kusafirishwa siku iliyofuata kwenda Bariadi na aliandika maelezo hayo ya ungamo.

Kuhusu maelezo yanayobishaniwa, wakili alisema Jaji alishughulikia hoja ya maelezo kuchukuliwa bila hiari na ushahidi wa mateso ambao mrufani aliuegemea katika utetezi wake, na kinacholalamikiwa kinapaswa kupotezewa.

Uamuzi wa jopo la majaji

Katika uamuzi wao, majaji wa Mahakama ya Rufani walisema hakuna ubishi kuwa Jaji aliyesikiliza kesi ndani ya kesi alikataa pingamizi la kutopokelewa kwa maelezo ya ungamo na kuhifadhi sababu akisema ataijumuisha kwenye hukumu yake.

“Hiyo pekee, ilikuwa inakiuka kanuni ya uamuzi wa kesi ya Jeneroza Petro dhidi ya Jamhuri ambayo tumeirejea kwamba sababu za uamuzi katika kesi ndani ya kesi lazima zitolewe kabla ya kesi kuu kuanza tena kusikilizwa,” walisema.

“Kama vile hiyo haikutosha, hata sababu zilizoelezwa zingetolewa katika hukumu. hazikuingizwa kwenye hukumu. Kwa maoni yetu kesi ndani ya kesi ni tofauti na kesi ya msingi. Njia aliyoitumia Jaji ilikuwa si sahihi,”walieleza na kuongeza kuwa:-

“Kupokea maelezo ya ungamo ambayo yanapingwa kama kielelezo P1 bila kueleza sababu za kuyapokea ilikuwa ni ukiukwaji wa taratibu na haikutenda haki na mrufani alinyimwa taarifa muhimu kupinga kesi ya Jamhuri,”walisisitiza.

Kutokana na dosari hizo walizozibaini, majaji hao wamesema sababu hiyo ya sita pekee inatosha kumaliza rufaa hiyo hivyo kutiwa hatiani kwa mrufani kunabatilishwa na jalada litarudishwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa upya.

Usikilizwaji huo utaanza pale ambapo upande wa utetezi ulifunga ushahidi wao katika kesi ndani ya kesi ili sasa Jaji mpya atakayepangiwa, atoe uamuzi wa kesi ndani ya kesi ndipo kesi ya msingi iendelee kwa mashahidi waliobakia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *