
Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Polycarp Kardinali Pengo, akieleza Taifa limepoteza kiongozi wa kiroho aliyetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi.
Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo alifariki dunia saa 4:00 usiku wa Februari 19, 2026 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikokuwa akipatiwa matibabu akiwa na miaka 82.
Katika barua yake kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Thaddaeus Ruwa’ich, Kikwete amesema msiba huo si wa Kanisa Katoliki pekee bali ni wa Watanzania wote.
“Nakuandikia kukufikishia salamu zangu za rambirambi kwa msiba mkubwa uliowapata kutokana na kifo cha Baba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Ni msiba wetu sote,” ameandika Kikwete.
Amesema wakati wa uhai wake na katika utumishi wake kwa kanisa, Kardinali Pengo alitoa mchango muhimu katika maendeleo ya nchi, huku akigusa maisha ya Watanzania wa rika na imani mbalimbali.
“Watanzania wengi wamenufaika, wakiwemo Wakristo na wasiokuwa Wakristo. Daima tutamkumbuka kwa mchango wake adhimu na kwa moyo wake wa upendo kwa wananchi wenzake na kwa nchi yetu pendwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alikuwa rafiki wa wengi,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Kikwete amemwombea Askofu Mkuu Ruwa’ich na waumini wote wa Kanisa Katoliki kuwa na moyo wa subira na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi, akisema anaungana nao pamoja na Watanzania wote kumuombea marehemu apate mapumziko mema.
“Naungana nanyi kumuombea mapumziko mema na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi. Amina,” ameandika Kikwete.
Kifo cha Kardinali Pengo kimeibua maombolezo makubwa nchini, huku viongozi wa dini, Serikali na wananchi wakieleza kuguswa na mchango wake wa muda mrefu katika uongozi wa kiroho na masuala ya kijamii nchini.
Katika taarifa yake mapema mwishoni mwa wiki, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kiongozi huyo wa kiroho, atazikwa Pugu Februari 28 mwaka huu.
Ratiba ya mazishi yake itaanza na kuwasili kwa mwili wake katika Kanisa la St Joseph kwa ajili ya misa itakayofuatiwa na maombi, hiyo ni Februari 27, 2026.
Desemba 24, 2025, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alitoa taarifa ya Kardinali Pengo kupelekwa nchini India kwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi wa kumpeleka kiongozi huyo wa kiroho nchini India ulitokana na kuugua kwa muda mrefu na matibabu yake kupangwa nje ya nchi.