
Tangu siku ya kwanza alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), kila mtu alijua kwamba ingefika siku Profesa Ibrahim Lipumba angeondoka kwenye hatamu. Hakuna aliyewaza mwisho ungekuwa wa aibu. Sasa, unaweza kulizoea jina, Mirambo Yusuf.
Uhai unapita, hata vyeo havina uzima wa milele. Kitu ambacho kinamfaa binadamu ni kutenda yaliyo mema ili ajenge athari chanya kwa vizazi.
Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliacha wosia katika nyakati za mwisho za uhai wake akisema:
“Maisha ya mwanadamu ni hadithi tu, basi huwa hadithi nzuri kwa hao watakaosimuliwa.”
Hadithi ya Lipumba CUF na katika siasa za Tanzania, ni kitabu cha wasifu wa shujaa aliyeimbwa na kuheshimiwa kwa matendo makuu ya kishujaa, lakini baadaye akajitengenezea mwisho uliofifisha ushujaa wake. Profesa Lipumba kutoka kuitwa mwalimu na nembo ya demokrasia, hadi kutafsiriwa kama bahati mbaya ya kisiasa.
Desemba 18 na 19, 2024, CUF walifanya mkutano mkuu, uliompa ushindi kuendelea kukalia kiti. Kundi moja la wana-CUF lililalamika kuwa ushindi wa Lipumba haukukidhi matakwa ya Katiba inayoelekeza mshindi wa uenyekiti sharti apate zaidi ya nusu ya kura za wajumbe wa mkutano huo.
Februari 13, 2026, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ilibatilisha matokeo ya uchaguzi ya CUF Desemba 2024.
Februari 21, 2026, uchaguzi wa marudio ulifanyika. Profesa Lipumba hakuchukua fomu ya kuomba kuchaguliwa tena. Matokeo yalipotangazwa, nafasi ya Mwenyekiti ikachukuliwa na Mirambo Yusuf.
Jina hilo kwenye kiti cha uenyekiti cha CUF, halina tafsiri nyingine zaidi ya mwanzo wa zama mpya za chama hicho, ambacho kiliongoza upinzani kwa muongo mmoja na nusu (1995 – 2010).
Februari 22, 2026, kwenye ukumbi wa Huntington Palace uliopo Washington Boulevard, Detroit, Michigan, Marekani, jumuiya ya Nationa Of Islam (NOI), walikuwa wanafanya kongamano kubwa la kukumbuka siku ya uzao wa mwasisi wa madhehebu yao, Wallace Fard Muhammad, ambayo huiita Saviours’ Day.
Kiongozi wa NOI, Louis Farrakhan hakuhutubia, badala yake alimpisha mwanafunzi wake, Ishmael Muhammad ahutubie.
Wakati akimtambulisha Ishmael kama mzungumzaji mkuu wa siku, Farrakhan alisema:
“Kiongozi mzuri hutambua vipawa vya anaowaongoza, ili waipokee kazi ya mwalimu mkuu. Mimi leo nakaa sehemu ya wasikilizaji. Mwanangu, nenda kafundishe.”
Maneno ya Farrakhan yanabeba ujumbe mchungu kuhusu zama. Uwe hodari wa fani yoyote muda ukifika, wahenga watajitokeza na kukwambia wakati ni ukuta.
Hivyo, kipindi unapokuwa unakwea kwenye umaarufu, ni muhimu kukumbuka kuna maisha mengine baada ya umashuhuri huo. Wenye kufanikiwa ni wale wanaoheshimu maneno ya gwiji wa sheria wa Kenya, PLO Lumumba, kwamba… “mchezaji mzuri hujua muda sahihi wa kushuka jukwaani.”
Lipumba hakujua muda wa kuondoka CUF, matokeo yake ameng’olewa kwa aibu. Hakutambua busara za Farrakhan kwamba kiongozi mzuri huandaa wanafunzi ambao huiendelea kazi.
Hiki ni kipindi ambacho, mmoja wa wale walioumizwa na uamuzi wa Machi 2009, Lipumba aliposhinda dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad (marehemu), sasa anaimba na kucheza.
Kipande cha marehemu Waziri Sonyo, akiwa na bendi ya TOT Achimenengule, ndicho kinamburudisha:
“Tulikusema hukusikia, asiyesikia la mkuu huvunjika guu na majuto mama aah, ni mjukuu.” Nyakati za mgogoro mkubwa wa CUF, baina ya Profesa Lipumba na Seif, tahadhari kubwa ilitolewa kwamba salama ya chama hicho ilikuwa Lipumba kuondoka kwa heshima. Hakutaka kusikia!
Profesa Lipumba alishauriwa kuwa nguvu ya CUF ilikuwa Zanzibar na kwa wakati huo, Seif ndiye alibeba uhai wa chama. Kila ushauri Lipumba hakutaka kuuelewa.
Aliweka pamba masikioni. Alichagua kubaki na CUF jina. Seif akahama na chama, akajiunga na ACT-Wazalendo. Mara, ACT – Wazalando ikawa ngome kuu ya upinzani Zanzibar na chama kinachotoa ahadi chanya Tanzania Bara. Profesa alibaki na CUF jina. Hatimaye, jina nalo limemkataa.
Naukumbuka mwaka 1995, Profesa huyo alipogombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kijana msomi ajabu kutoka Ilolanguru, Tabora. Mchumi mbobevu. Wana-CUF wakampenda, wakamwamini. Wakamchagua kuwa mwenyekiti.
Kuanzia hapo akawa lulu ya kisiasa na kivutio cha wengi. Kuna wanasiasa wengi leo katika siasa za mageuzi, ama walivutiwa naye au walijengeka kutokana na harakati zake.
Mwaka 1995 alitoka wa tatu, mbio za urais. Mwaka 2000, alishika nafasi ya pili. Hiki ndicho kipindi cha Lipumba katika kimo chake kikuu kisiasa.
Namkumbuka Profesa Lipumba wa mwaka 2001. Lipumba mwenye ari ya kupambana, mwenye kuikabili misukosuko ya kisiasa bila hofu wala kurudi nyuma. Lipumba mwenye moyo mkubwa kwa CUF, wanachama wake na nchi yake Tanzania.
Baada ya maandamano ya Januari 26 na 27, 2001, Zanzibar na Dar es Salaam, CUF wakitaka watangazwe washindi wa Uchaguzi Mkuu 2000 na Seif atamkwe ndiye Rais wa Zanzibar, machafuko ya kihistoria yalitokea.
Wazanzibari wengi walipoteza maisha, maelfu walijeruhiwa na hata kupata ulemavu. Aibu kubwa zaidi ikawa kwa Tanzania kutengeneza wakimbizi waliokimbilia Mombasa na Lamu, Kenya. Kuna ambao walifika mpaka Somalia.
Lipumba akiwa anaongoza maandamano kwa Dar es Salaam, alikamatwa, alipigwa, alijeruhiwa na hata kuteguka mkono. Na akiwa na majeraha yake, aliwekwa mahabusu pamoja na wanachama, vilevile wafuasi wengine wa CUF.
Hii ni kuonesha kuwa yeye ni mwenyeji wa dhoruba za siasa za mageuzi kuliko wengi wanaoamini wameingia gharama kubwa kudai demokrasia. Gharama ambayo Lipumba ameilipia kwenye siasa za vyama vingi nchini haina fidia.
Wakati kesi ikiendelea mahakamani, dhamana ikawa wazi kwake ili apate fursa ya kutibiwa. Hata hivyo, aligoma kutoka mahabusu kwa maelezo kuwa angekuwa wa mwisho kupata dhamana.
Kwa msisitizo alisema kuwa watu wote waliokamatwa katika vurugu za Januari 26 na 27, wakishapata dhamana ndipo yeye atatoka. Wakati akiumwa, akiteseka kwa kukosa uhuru, lakini akawa anafikiria uhuru wa wengine kwanza.
Kwa umri wake, uungwana na gharama ambayo ameilipa kwa siasa za nchi hii, hakika alihitaji nishani za demokrasia na uhuru. Yote yanaweza kusemwa, lakini haisahauliki nyakati zile ambazo upinzani ulipozungumzwa, jina la Lipumba lilisogea haraka mawazoni.
Lipumba alikuwa jina kuu, kipindi CUF ikiwa chama kikuu cha upinzani, na kilipelekana puta na dola. Tambo za ngangari na sera za utajirisho. Chama kilikuwa na wimbo wake (party anthem), na wafuasi wake waliimba kwa fahari kubwa.
Hotuba za Profesa Lipumba, zilichapwa kwenye magazeti. Watu walimpenda, walimtukuza na kumpamba kwa sifa kemkemu. Lipumba alikuwa kinara wa upinzani, CUF ilibeba matumaini ya wapinzani.
Chadema ni chama chenye ufuasi mkubwa hivi sasa, mwaka 2000, hakikusimamisha mgombea urais, karata yao waliiweka kwa Lipumba. Ni bahati mbaya Lipumba amejitengenezea anguko mwenyewe.
Mwaka 2015, Lipumba alijiuzulu uenyekiti CUF. Alikwenda kukaa Rwanda kupisha Uchaguzi Mkuu 2015.
Aliporejea, akaandika barua ya kutengua kujiuzulu kwake. Akataka kurejea kwenye kiti. Msajili alimthibitisha Lipumba. Kesi ilipokwenda mahakamani, Lipumba alishinda. Seif na timu kubwa ya viongozi na wanachama wakahamia ACT – Wazalendo.
Uchaguzi Mkuu 2020 na 2025, ulikuwa kipimo kwamba CUF imebaki jina. Mikutano yake ya hadhara haikuwa na msisimko, na mahudhurio yalikuwa kidogo.
Kwa yeyote mwenyewe, angejisikia vibaya kuona chama ambacho kilipata kuisimamisha nchi kwa miaka 15, kiliporomoka na kulingana na vyama vidogo ambavyo havijawahi kutengeneza historia yoyote katika safari ya demokrasia.
‘My political party is not my religion and it shouldn’t be yours either.’ – “Chama changu cha siasa siyo dini yangu na hakipaswi kuwa dini yako pia.”
Pengine maneno hayo ya Waziri Mkuu wa zamani wa Canada, Mackenzie King, yanaweza kumfariji Lipumba. Tusisahau, mwandishi Eddie Stone aliandika: “What comes around goes around.”