
Zaidi ya kaya 2,500 zimeachwa bila makazi baada ya mito miwili kuvunja kingo zake na kusababisha mafuriko katika vijiji kadhaa katika eneo la kati, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mvua kubwa iliyonyesha hivi karibuni katika jimbo la Maniema imesababisha Mto Kongo na Mto Ulindi kufurika na kulazimisha mamia ya watu katika vijiji vya Kasera, Tubila na Ulindi kuhama makazi yao. Haya yameelezwa na Jean-Claude Ngoy, Mkuu wa Shirika la Kiraia katika eneo la Punia.
Ameongeza kuwa, kaya zisizopungua 2,533 zimeathirika baada ya nyumba zao kuzamishwa na maji. “Tunaziomba mamlaka za jimbo na kitaifa pamoja na wahusika wa misaada ya kibinadamu kutusaidia,” amesema Ngoy.
Mafuriko yaliyovikumba vijiji vya Kasera, Tubila na Ulindi katika jimbo la Maniema nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yameharibu na kubomoa miundombinu, zikiwemo shule, vituo vya afya na vyanzo vya maji ya kunywa.
Timu ya tathmini inayoundwa na mamlaka za mitaa, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na viongozi wa jamii imeeleza kuwa raia walioathiriwa na mafuriko wanaweza kukabiliwa na njaa kwa sababu mashamba yao ya chakula na mabwawa ya samaki yamefurika maji.