VIONGOZI wa masoko mkoani Dar es Salaam wamesema kupanda au kushuka kwa bei ya vyakula kunategemea zaidi upatikanaji wa bidhaa husika sokoni.
Mwenyekiti wa soko la vyakula la Temeke Stereo wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam, Rashid Milao amesema katika soko hilo bei za mazao zikiwemo ndizi, viazi na magimbi hubadilika kulingana na wingi au uhaba wa bidhaa unaotokana na msimu wa uzalishaji na usafirishaji kutoka mikoani.
Milao amesema kwa kawaida kipindi cha kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani mahitaji ya vyakula huongezeka kwa kuwa familia nyingi huandaa futari na daku kila siku. Ndizi, viazi, magimbi na viazi vitamu ni miongoni mwa vyakula vinavyotumika zaidi katika kipindi hicho.
Milao amesema katika soko hilo, bei za vyakula hazipandi kwa sababu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani pekee bali hutegemea upatikanaji wa bidhaa. “Zikipatikana kwa wingi hata kama mahitaji ni makubwa bei hubaki vilevile. Tatizo linatokea pale ambapo mahitaji yanaongezeka lakini mzigo unaoingia sokoni ni mdogo,” alisema. SOMA: Mageuzi kulibeba Soko la Kariakoo

Milao amesema watumiaji wa nazi hawataathiriwa na ongezeko la bei kwa kuwa msimu huu wa mfungo umekuja sanjari na msimu wa nazi ambazo zinapatikana kwa wingi sokoni hapo kwa bei ya kuanzia Sh 500 kwa nazi moja. Wafanyabiashara katika soko hilo wamesema ongezeko la magari ya mizigo litasaidia kuleta ushindani miongoni mwa wauzaji hivyo bei za bidhaa, ikiwemo vyakula, zitashuka au zitatulia.
Wamesema kuwa changamoto ya gharama za usafirishaji huchangia kupanda kwa bei hasa ya mafuta inapoongezeka au barabara zinapokuwa katika hali mbaya wakati wa mvua. Ofisa Kilimo katika soko la Mabibo wilayani Ubungo, Pavelina Chitanda amesema katika siku za karibuni bei ya viazi mviringo katika soko hilo imepungua kutoka Sh 130,000 hadi Sh 80,000 kwa gunia.
Chitanda amesema mkungu wa ndizi unauzwa kati ya Sh 25,000 hadi Sh 50,000 kutegemeana na aina na ukubwa wa mkungu husika. Amesema magimbi hayajaanza kupatikana kwa wingi katika soko hilo na bei yake ya jumla ni kati ya Sh 80,000 hadi Sh 120,000 kwa gunia.