Dar es Salaam. Mwanaume mmoja aliyekuwa amebeba silaha ameuawa kwa kupigwa risasi na maofisa wa usalama baada ya kukaribia eneo la makazi ya Rais wa Marekani, Donald Trump, katika jimbo la Florida.

Tukio hilo limethibitishwa na Idara ya Usalama wa Rais Trump, ambayo ilisimamia operesheni ya kumdhibiti mtuhumiwa huyo.

Mashirika ya habari ya kimataifa kutoka nchini humo yakiwemo BBC na DW, yanaripoti kuwa mwanaume huyo alikuwa amebeba bunduki pamoja na kopo la mafuta alipokaribia eneo hilo lenye ulinzi mkali.

Inaelezwa maofisa wa usalama walimwamuru asimame na kuweka chini silaha alizokuwa nazo, lakini inadaiwa alikataa kutii amri hizo hivyo iliwalazimu kutumia nguvu ikiwamo kumpiga risasi.

Tukio hilo limetokea Jumapili Februari 22, 2026 ambapo inaelezwa Trump hakuwepo Florida, bali alikuwa Washington DC.

Vyanzo vya usalama nchini humo vimeeleza kuwa hakuna majeruhi wengine walioripotiwa katika tukio hilo, na hatua zilizochukuliwa zililenga kuzuia hatari inayoweza kutokea kwa watu na mali zilizokuwa katika eneo hilo.

Mshukiwa huyo aliyeuawa ametajwa kwa jina la Austin Martin, mkazi wa Cameron, North Carolina.

Taarifa zinaeleza familia yake ilikuwa imeripoti, “alitoweka mapema Jumapili asubuhi, kabla ya tukio hilo kutokea” huku Ofisi ya Polisi ya eneo la Moore, North Carolina, ikithibitisha kupokea taarifa hizo za familia.

Idara ya Usalama imeeleza kuwa hadi sasa hakuna historia ya uhalifu inayohusishwa na Martin.

 Bado uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo chake na kama kulikuwa na nia yoyote ya kushambulia au kusababisha madhara zaidi.

Maofisa wa usalama wamesisitiza kuwa wataendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote yanayohusiana na viongozi wa kitaifa, huku wakitoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema pale wanapobaini mienendo ya kutia shaka.

Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu usalama wa viongozi wa juu wa Marekani hasa kutokana na historia ya tukio la miaka miwili iliyopita dhidi yake, pamoja  na harakati za Rais Trump ambazo amekuwa akizichukua zikizua mijadala ya kimataifa.

Julai 2024, Trump alipigwa risasi sikioni alipokuwa amesimama mbele ya umati wa watu huko Butler, Pennsylvania.

Moja ya matukio yaliyotikisa dunia yakimuhusisha Rais Trump ni pamoja na uvamizi wa Taifa lake nchini Venezuela na kumnyakua Rais wake ambaye mpaka sasa anashikiliwa Marekani.

Zingine ni tamko lake la kukitwaa kisiwa cha Greenland pamoja na vikwazo vya kikodi kwa mataifa ya Ulaya ambayo hayakubaliani na msimamo wake huo.

Mbali na Ulaya, Rais Trump ameweka vikwazo vya kuingia Marekani kitalii, kimasomo, kimatibabu na kimabadilishano kwa mataifa mengi ya Afrika na ya nchi za Kiarabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *